The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi Walivyofundishwa Jinsi Ya Kupambana Na Ukatili Wa Kijinsia

0
Erick Anderson kutoka Kikundi cha Taarifa na Maarifa cha Kivule akisoma risala.

Dar es Salaam 6 Desemba 2023: Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bombambili iliyopo eneo la Bombambili Kata ya Kivule Wilaya ya Ilala jijini, leo wamefundishwa namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya siku 16 za kupinga ukatili duniani.

Wanafunzi hao wamepata elimu hiyo kutoka kwa wanaharakati wa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) cha Kata ya Kivule kilichopo chini ya Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP).

Katika mafunzo hayo mgeni rasmi alikuwa Mwalimu Siwema Makene aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Kata ya Kivule ambapo alikipongeza kikundi hicho kwa kupeleka elimu hiyo kwenye wanafunzi wa kata yake pamoja na kuibua changamoto mbalimbali kwenye kata hiyo.

Mwalimu Siwema Makene aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Kata ya Kivule.

Kwa upande wa uongozi wa shule hiyo uliwakilishwa na Mwalimu Sekela Boniface ambaye alikishukuru kikundi hicho kilichopo chini ya TGNP kwa kupeleka mafunzo hayo kwenye shule hiyo ambayo imeshakumbana changamoto za watoto kufanyiwa ukalitili wa kijinsia mara kadhaa.

Mwalimu Sekela amesema watoto baada ya kupata mafunzo hayo sasa wameshaondolewa hofu na kuelekezwa namna ya kuyaripoti matukio hayo na kutajiwa namba 116 ambayo watatakiwa kupiga bila woga endapo watahisi kufanyiwa ukatili wa kijinsia kama vile kupigwa vipigo visivyo vya kawaida, kushawishiwa kufanya ngono na mengineyo. Aliendelea kusema;

Mmoja wa wanafunzi akielezea alichokielewa kwenye mafunzo hayo.

“Watoto wengi hapo awali ilikuwa unamkuta tu mtoto amepooza ghafla tofauti na siku za nyuma na ukijaribu kumdodosa wengi walikuwa waoga kusema ukweli kwa kuwaogopa watu wanaowafanyia vitendo hivyo labda mpaka umbane sana ndiyo atakuambia, sasa elimu itasaidia sana kupunguza changamoto hiyo baada ya kuwapa watoto hawa ujasiri wa kuripoti matendo hayo”.

Picha ya pamoja ya wanafunzi, walimu, viongozi wa Serikali ya Mtaa na Wanakikundi cha Taarifa na Maarifa Kivule.

Kwa upande wake Erick Anderson kutoka Kikundi cha Taarifa na Maarifa cha Kivule akisoma risala yake kwa mgeni alisema kikundi hicho kimeibua ukatili mwingi sana wa kijinsia ambapo kwasasa hali ni tulivu kiasi baada ya nyingi kuziwasilisha kwenye vyombo vya sheria na kufuata mkondo.

Wanafunzi wakishangilia baada ya mafunzo hayo.

Ameendelea kusema Erick kuwa kikundi hicho kitaendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia hata baada ya siku hizi 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ulimwenguni kupita. HABARI/PICHA NA RICHARD BUKOS WA GLOBAL PUBLISHERS

Leave A Reply