The House of Favourite Newspapers

WANAFUNZI WANNE WAFARIKI MBELE YA WALIMU

DAR ES SALAAM: Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kimbiji, Kingamboni jijini Dar es Salaam; Celestina Malipesa (18), Agneta’s Philipo (18), Cesilia Ernest (17) na Qeen Mandala (17) wamefariki baada ya kuzama kwenye maji walipokuwa wakiogelea baharini.

 

Tukio hilo limetokea Jumamosi iliyopita katika ufukwe wa Chanza Mwamba wakati wanafunzi hao walipokuwa na wenzao wanaotarajia kumaliza kidato cha nne walipokwenda kujipongeza ufukweni huku wakijiandaa na mtihani wa kuhitimu. Akisimulia tukio hilo, mmoja wa shuhuda, alisema wanafunzi hao walifanya vizuri kwenye mtihani wao wa Mock hivyo wakashauriana na walimu wao, waende kujipongeza.

 

“Waliaandaa vyakula vyao pamoja na vinywaji, wakaenda kujipongeza ‘bichi’. Walipofika huko wakaanza kucheza michezo mbalimbali chini ya uangalizi wa walimu wao,” alisema shuhuda huyo.

Alisema, wanafunzi wa kiume, walikuwa wakicheza mpira kandokando ya bahari na wasichana walikuwa wanacheza upande wao mpira wa netiboli. “Sasa mwalimu akawa anawaangalia zaidi wanafunzi wa kiume kuliko hawa wa kike sababu aliamini ndiyo wakorofi na wanaohitaji uangalizi wa karibu.

 

“Kuna wakati mpira wa wale wanafunzi wa kike ukaingia kwenye maji. Huyu Selestina alikwenda kwenye maji kuufuata, maji yakawa yanamzidi hivyo akaanza kuomba msaada, sasa wenzake hao watatu wakamfuata kwenda kumuokoa ndipo walipojikuta wamezama wote,” alisema shuhuda huyo.

 

Akizidi kusimulia shuhuda huyo, alisema, wakati tukio hilo likitokea, baadhi ya wanafunzi wa kiume walitaka kwenda kuwasaidia lakini walimu wao walilazimika kuwazuia kwa kuhofia maafa zaidi. Baada ya jitihada za wasamaria wa Mtaa wa Kwa Charle kufanyika, walifanikiwa kuwaopoa watoto hao wakiwa tayari wameshafariki.

 

Mwenyekiti wa mtaa huo Silvery Salikisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na zaidi aliwaasa wananchi kuwa makini wanapokuwa ufukweni kwani mara kwa mara watoto wamekuwa wakienda ‘bichi’ kuogelea bila kuwa na tahadhari ya wazazi.

 

“Niwasihi wazazi wanapokuwa na watoto wao ufukweni wawe makini maana wakiwaacha tu wenyewe matatizo kama haya yanaweza kutokea,” alisema mwenyekiti huyo. Mwili wa Selestina ulizikwa katika makaburi ya juzi Jumatatu huku wenzake wakiendelea kufanyiwa utaratibu wa mazishi na ndugu zao.

STORI: Neema Adrian, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.