The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi Watatu Nchini Kenya Wafa Mtoni Wakifua Sare za Shule

0
Wanafunzi wamefia kwenye mto wakiwa wanafua sare za shule

WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi Gakuyu wamefariki dunia katika Mto wa Kathita, Kaunti ya Tharaka Nithi, nchini Kenya wakati wapokwenda kufua sare zao za shule, juzi Jumamosi, Septemba 24, 2022.

 

Wanafunzi hao wenye umri wa miaka ya 13, 12 na 10 walikuwa wametembea kilomita kadhaa kutoka Kirikuma hadi kata ndogo ya Gituma wakitafuta maji ya kufua sare zao kabla ya kukumbwa na umauti huo.

 

Chifu wa Gituma, Kibaara Muthungu, alisema watoto hao mmoja akiwa mtahiniwa wa darasa la nane walikuwa wakijaribu kuvuka mto hadi mahali ambapo wangeweza kufua sare zao ndipo wakazama.

 

Muthungu aliongeza kuwa mtoto mmoja ambaye alinusurika kifo ndiye alipiga kelele kuwavutia majirani wa eneo hilo ambao walikimbia katika eneo la tukio lakini tayari watatu hao walikuwa wamepoteza maisha yao.

 

Miili ya watatu hao ilichukuliwa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Marimanti Level Four.

 

Chifu msaidizi wa Gituma, Josphat Muriungi alisema watoto wawili kati ya waliofariki walikuwa ndugu. Alisema kutokana na ukame unaoendelea kukumba kaunti hiyo na kusababisha kukauka kwa mito mingi inayotiririsha maji mwaka mzima, wakazi wanasafiri mbali kutafuta maji, kufua nguo na kunywesha mifugo yao katika Mto Kathita au Mto Tana.

 

Aliongeza kuwa wakazi wa maeneo mengi ya eneo Bunge la Tharaka wanateseka kutokana na ukosefu wa maji na baa la njaa hivyo akaiomba serikali kuwapatia maji ya bomba kama suluhu ya kudumu.

 

Kulingana na Muriungi shule pia zinatarajiwa kuathirika kutokana na uhaba wa maji na kuitaka serikali ya kaunti kutafuta suluhu la haraka.

 

“Mito kadhaa ya kudumu na ya msimu hupitia eneo letu ikiwa ni pamoja na Mto Tana lakini watu bado wanateseka kwa ukosefu wa maji isipokuwa wale walio karibu na mito ambao pia wako katika hatari ya kuzama au hata kushambuliwa na mamba au viboko,” alisema Muriungi.

 

Takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 38,517 katika sehemu zenye ukame za eneo bunge la Tharaka wanahitaji msaada wa chakula na maji.

Leave A Reply