The House of Favourite Newspapers

Wanafunzi Watekwa, Basi Lao Lachomwa Moto

 

BASI lililokuwa limebeba watoto wa shule wapatao 51 lilitekwa na kutiwa moto karibu na jiji  la Milan nchini Italia.

 

Watoto hao wa shule, ambao baadhi yao walifungwa kamba, waliokolewa baada ya kuvunjwa vioo vya basi hilo upande wa nyuma na hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa vibaya.    Watu kumi na wanne waliathiriwa na moshi uliotokana na kuteketea kwa basi hilo.

 

Dereva wa basi hilo alikuwa na umri wa miaka arobaini na saba mwenye uraia wa nchini Italia ingawa ana asili ya kutoka nchini Senegal, inaarifiwa kwamba ametiwa nguvuni.

 

Dereva huyo alisikika akitamba, akiwaambia waliokuwemo katika basi hilo kwamba hakuna hata mtu mmoja atakayenusurika.  Ulikuwa ni muujiza, vinginevyo yangekuwa ni mauaji ya halaiki, alinukuliwa akisema hayo mwendesha mashtaka mkuu wa mjini Milan aitwaye Francesco Greco.

 

Mwalimu mmoja aliyekuwa ndani ya basi wakati tukio hilo likitekelezwa, alimwelezea mtuhumiwa huyo kuwa alikuwa na silika ya hasira mara kwa mara na kubwa hasa ni juu ya sera za wahamiaji nchini Italia.    Taarifa zingine zinaarifu kuwa dereva huyo alisikika akibwata akisema kwamba “sitisheni mauaji katika bahari ya Mediterranean”.

 

Makundi mawili ya wanafunzi waliokuwa wakisindikizwa na walimu wao, walikuwa wameyatoka mazingira ya shule iitwayo Vailati di Crema wakielekea kwenye mazoezi lakini baadaye gari ikachukua mwelekeo tofauti na safari yao na kuelekezwa kwenye barabara kuu ya mkoa na kufuata njia inayoelekea katika uwanja wa ndege wa Milan Linate, ripoti za mashuhuda zinaarifu.

 

Suala hilo liling’amuliwa dakika arobaini baadaye, wakati dereva alipowaelekezea abiria wake kisu huku akizungumza maneno.  Wakati huohuo, mvulana mmoja aliwapigia simu wazazi wake kwa siri, ambao nao waliwafahamisha polisi juu ya tukio hilo.

 

Ilichukua muda kidogo kabla polisi hawajalifikia basi lililotekwa na kujaribu kulifanya lisimame,na mara basi hilo lilianza kulibamiza gari la polisi kabla ya kupunguza mwendo na kusimama kabisa.

 

Taarifa kutoka nchini Italia zinaarifu kuwa mafuta ya petroli yalinyunyizwa kulizunguuka basi hilo la shule, lakini polisi walitumia mbinu ya kuvunja madirisha ya nyuma ya basi hilo na hivyo kuwaruhusu abiria kushuka kwa haraka kabla basi hilo halijalipuka kwa moto.

 

Waendesha mashitaka wa Milan waliasema wanafanya uchunguzi wa kina kama kulikuwa na nia zozote mbaya ikiwa ni pamoja na ugaidi.    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Matteo Salvini, alizungumza kwa hasira kwamba dereva huyo alikuwa na rekodi ya uhalifu.

Comments are closed.