Wakinukisha Baada ya Kuporwa Fedha na Sungusungu

KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Carolius Misungwi,  ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Sungusungu katika kata ya Mfinga iliyopo bonde la ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga kufuatia Sungusungu hao kuzua taharuki baada ya kuwazuia wanakiijiji kuendelea na shughuli zao na kuwakusanya uwanjani na kuwanyang’anya fedha pamoja na kutoa adhabu kwa waliogoma kutii amri zao.

 

Misungwi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya amemuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Sumbawanga  na Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya kuhakikisha wanafika katika kijiji hicho na kukutana na uongozi wa Sungusungu wa Kata na wa Kijiji ili kuwapa elimu juu ya namna ya kufanya shuguli za ulinzi shirikishi kwa taratibu zinazokubalika kisheria na si kujichukulia sheria mkononi.

 

“Kuanzia leo nimesimamisha shughuli zote za Sungusungu mpaka atakapokuja OCD kutoa mafunzo ya namna ya kufanya ulinzi shirikishi, na tungependelea sana kuwa na polisi jamii kuliko kuwa na Sungusungu, Sungusungu hawa hawa watapewa mafunzo watakuwa polisi jamii, haya mambo ya kutoza hela na kunyang’anya simu yatakuwa ndiyo mwisho wake, na wale wote waliotozwa fedha kinyume cha sharia watarudishiwa fedha zao,” alisema.

 

Maagizo hayo ameyatoa baada ya kusikiliza vilio kadhaa vya wananchi wa Kijiji cha Mfinga na Msila katika kata ya Mfinga Wilayani humo, baada ya wanakijiji hao kupatwa na sintofahamu baada ya kundi la Sungusungu kuvamia vijiji hivyo na kupora fedha za wanakijiji hao na kupelekea taharuki kusambaa hali iliyowakatisha wananchi kushiriki katika kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 28.10.2020.

 

Mmoja wa wanakijiji cha Msila Mashaka Lupondeja alisema kuwa Sungusungu hao walikuwa wanawalazimisha watu kutoa fedha bila ya utaratibu wowote huku wakiwatishia kwa majambia, jambo ambalo liliwakatisha tamaa wakidhani kuwa serikali haipo upande wao na kuwa serikali ndiyo imewatuma wanyang’anyi hao.

 

Nae Amour Mohamed wa Kijiji cha Mfinga alisema, “Mtendaji wa kata ndio anajua lile kundi lililopiga watu hapa, na sio leo tu huu ni mwaka wa tatu sungusungu wamechukua hatamu hapa kata hii, viongozi wapo hawataki kuchukua hatua, mwananchi anatozwa mpaka milioni sita, anaambiwa usipolipa tunakuua na watu wanakufa, mi nashangaa uongozi wa Kijiji na wa kata kigugumizi gani wanapata, uwaulize mbele ya mkutano huu”.

 

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Msila wakati akielezea tukio la Sungu Sungu hao kuwakusanya wakazi wa kijiji hicho uwanjani na kuwapora fedha alisema kuwa, uongozi wa Sungusungu uliofanya hivyo umetoka ngazi ya tarafa kuja kwenye kijiji hicho na kubainisha kuwa kulitokea na kutoelewana baina ya uongozi wa Sungusungu wa kijiji na tarafa hatimaye wananchi wote kuhusishwa katika sakata hilo kwa kukusanywa uwanjani.

 

 

Toa comment