The House of Favourite Newspapers

Wanangu, Mapenzi, Mtayakuta Mtayakinai

0

Couple-in-BedJamani leo nimekaa na kujiuliza mambo mengi kuhusiana na maisha tunayoishi hivi sasa, wazazi tumekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili kutokana na kuwaacha watoto wao wafanye watakavyo kwa kuamini tunakwenda na wakati.

Unatembea mtaani unakutana na wasichana mavazi na nywele zao zilivyo timutimu utaamini kabisa wamekosa malezi ya maadili ya kike.

Wazazi leo hii mnashangaa mtoto kufeli vibaya, kama hatutashtuka basi mwisho wa watoto wetu utakuwa kidato cha nne.

Kwa vile kazi yangu kujenga, naomba leo nichukue nafasi ya wazazi wenu, nizungumze na ninyi wari wangu mnaojiita kizazi cha dotikom. Najua hiki ninachokizungumza kama hukukisoma basi mama yako atakwambia.

Mwari wangu, elimu inaanzia nyumbani, malezi yakiwa mazuri hata maendeleo katika maisha yako yatakuwa mazuri ikiwemo shuleni. Siku zote unavyojiweka ndivyo hukujenga katika picha yako halisi japokuwa wapo wanaosema eti umbile la nje ni tofauti na moyo wa mtu, si kweli nje na ndani huwa sawa.

Siku zote unavyojiweka ndiyo unavyosomeka, zamani wakati sisi tunakua, ilikuwa ajabu kumuona msichana amevaa suruali. Tulimheshimu kila mtu, wenye umri wa baba zetu tuliwaita baba na wenye umri wa kaka zetu tuliwaita kaka au dada.

Tuliishi kwa kuogopa kunyooshewa vidole kuwa tuna tabia mbaya, kila aliyeonekana ana tabia mbaya tulikatazwa kuwa naye karibu kwa kuhofia utaambukizwa tabia mbaya.

Tulichunga midomo yetu hatukuwa watu wa kusema maneno machafu, hatukujichanganya na watoto wa kiume kwa vile wanawake tuna vitu vyetu vya siri.

Pamoja na kusoma shule za kawaida tulizingatia masomo, japokuwa enzi zetu kwenda sekondari ilikuwa mbinde,  shule nzima anashinda mwanafunzi mmoja, siyo siku hizi anafeli mmoja darasa zima wanafaulu.

Hivi sasa katika watoto mia utakuta watano tu ndiyo hawajaanza mapenzi, lakini kila mmoja ana mpenzi pengine zaidi ya mmoja.

 Kuingia kwenye mapenzi katika umri mdogo ni somo lingine tofauti na la darasani, kwani mapenzi kwa wasichana wadogo ni somo lenye majibu mepesi ambalo halihitaji kupoteza muda kusoma usiku wa manane kuhifadhi majibu kwa kuandika kwenye sketi.

Somo hili majibu yake yapo wazi kama hukupata mimba basi maambukizi ya VVU, huko kote ukivuka salama basi unaugua ugonjwa wa hisia za mapenzi kwa kutaka kila wakati kwa vile sigara ya kuokota aishi hamu na siku zote kusinzia kutamu kuliko kulala.

Mapenzi ya wizi ya kuogopa kuchelewa nyumbani matamu kweli.

Somo hili limekuwa likichukua nafasi katika akili za wasichana wengi kufikia hatua ya kuwafanya waote mapembe na kusahau mapenzi yapo na yana wakati wake. Soma kwa bidii na ukimaliza utaolewa.

Hebu wazazi tuchukue nafasi zetu na nyinyi wasichana jitambueni, usikimbilie mapenzi kwa kuamini mmekua na kupoteza fedha za wazazi wetu. Muonee huruma mzazi wako ili kujijengea maisha, yangu leo yanatosha.

 

Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

Leave A Reply