The House of Favourite Newspapers

Wajeruhiwa kwa kuvamia Kituo cha Polisi Moro

0

SILAHA

Watu wanne wamejeruhiwa kwa risasi na Polisi mkoani Morogoro wakati wakijaribu kuvamia kituo cha Polisi cha Dutumi kilichopo Wilaya ya Morogoro kwa nia ya kuwakomboa wenzao waliokamatwa kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe.

Imeelezwa kuwa zaidi ya watu 30 wakiwa na silaha za jadi walijaribu kuvamia kituo hicho cha Polisi na kujaribu kuwakomboa wenzao hata hivyo jaribio hilo liliweza kuzimwa na Jeshi la Polisi mara baada ya kutumia risasi za baridi na moto katika kuwazuia na kufanikiwa kuwashikilia watu watatu.

Kisa cha wananchi hao kuvamia kituo hicho, ilikuwa ni kutaka kuwaokoa watuhumiwa watatu waliokuwa wakishikiliwa na jeshi hilo, mara baada ya kuiba ng’ombe sita.

Hata hivyo juhudi hizo ziliweza kugonga mwamba mara baada ya jeshi la Polisi kuamua kutumia nguvu za ziada kuwazuia wananchi hao kutekeleza kusudio hilo la kuvamia kituo cha Polisi Dutumi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ASSP Graifton Mushi ametoa onyo kwa wale wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na taratibu.

Jeshi la Polisi mkoani hapo linaendelea kuwasaka wale wote waliohusika na tukio hilo, na pindi watakapotatikana watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Credit: Star TV

Leave A Reply