The House of Favourite Newspapers

HAWA WASAFI BANA, TABU TUPU MTWARA – VIDEO

LILE tamasha la muziki la kukata na shoka la Wasafi Festival, limeacha balaa tupu mjini Mtwara, Ijumaa Wikienda ni shuhuda namba moja.

 

Kabla ya shoo baab’kubwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona usiku wa kuamkia jana, Wasafi chini ya bosi wao, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ walisababisha matukio mengi ambayo yaligeuka gumzo. Kabla ya shoo hiyo, timu nzima ya wasanii, wanahabari na mashabiki ilitinga kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa kwa ajili ya kupata baraka zake za kiusalama za kufanikisha tukio hilo.

 

 

Wakiwa kwenye ofisi hizo, Diamond alimwaga misaada ya mamilioni kwa ajili ya vifaa vya shule za msingi kwa wanafunzi 100 zikiwemo sare, wino, kalamu na madaftari kabla ya kuwasaidia mitaji walemavu wapatao 100 mbele ya mkuu huyo wa mkoa.

 

MATUKIO YA VICHWA VYA HABARI

 

Baada ya hapo sasa ndipo yakajiri matukio mengine yenye kutengeneza vichwa vya habari ikiwa ni pamoja na kitendo cha Diamond kulizwa cheni zote alizokuwa amevaa shingoni zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 40 za Kitanzania.

 

Matukio mengine ni pamoja na dansa wa Wasafi Classic Baby (WCB), Moses Iyobo kudaiwa kutibuana na mkewe ambaye ni staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel. Ukiacha matukio hayo na mengine, lingine ni lile la waliokuwa wapenzi zamani, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na mwigizaji Jacqueline Wolper kumaliza tofauti zao kisha kugandana kimahaba.

DIAMOND KULIZWA

Katika tukio hilo, Diamond alikuwa akikatiza mitaani mjini Mtwara baada ya kufika muda wa jioni kuelekea usiku huku akisalimiana na mashabiki wake akiwa amening’nia kwenye mlango wa gari ndipo akakutwa na janga hilo.

 

 

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani Mtwara lilifanya kazi yake ya kumtia mbaroni shabiki aliyefanya tukio hilo na kuapa kula sahani moja na mhalifu huyo. Akizungumza na Ijumaa Wikienda juu ya tukio hilo, Diamond alisema cheni hizo ni za madini aina ya Almasi, Dhahabu na Tanzanite na kwamba gharama yake ni zaidi ya shilingi milioni 40 kwa zote tatu.

 

“Kwanza nilishtuka maana siyo pesa ndogo. Ni madini mchanganyiko. Kulikuwa na Almasi, Dhahabu na Tanzanite. “Kama binadamu imeniuma sana, lakini huwezijua inaweza ikawa kumbukumbu nzuri kwake kwamba naye aliwahi kukutana na kushikana na Diamond,” alisema jamaa huyo.

 

 

AUNT NA IYOBO

Katika tukio lingine kubwa, Aunt na Iyobo walizua sintomfahamu baada ya kudaiwa kufikia hoteli tofauti na kuwa wanapishana bila kusalimiana. Kufuatia hali hiyo mmoja wa watu wa ndani wa Wasafi aliling’ata sikio Ijumaa Wikienda kuwa, wawili hao hawakuwa sawa kwani walikuwa wametibuana.

 

Hata hivyo, baada ya wawili hao kuwekwa chini na watu wazima waliokuwa kwenda msafara huo, wawili hao hatimaye walionekana pamoja katika mapozi ya kimahaba, hali iliyoonesha mambo kukaa sawa huku wakionekana wakiongea kwa muda mrefu.

 

 

Kama desturi yake, Ijumaa Wikienda lilimfikia Iyobo na kuzungumza naye juu ya kutibuana na Aunt, lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo. “Nani amesema tumetibuana? Siwezi kuongelea hilo tafadhali ni mambo binafsi na yatabaki hivyo,” alisema Iyobo na kuondoka mbele ya mwandishi wetu. Kwa upande wake, Aunt aliomba asizungumze chochote juu ya jambo hilo.

 

WOLPER NA HARMONIZE

Baada ya kupita kwa zaidi ya mwaka mmoja wakiwa hawazungumzi tangu walipoachana, kwa mara ya kwanza, Wolper na Harmonize walionekana pamoja huku wakigandana kwa kukumbatiana.

 

 

Ilikuwa ndani ya hoteli waliyofikia hapa Mtwara ya Naf Beach ambapo Harmonize alipofika alisalimia na watu wote kisha kwenda kumkumbatia Wolper na kusababisha kelele nyingi kutoka kwa mashabiki wa Harmonize waliojazana hotelini hapo. Kama hiyo haitoshi, mashabiki hao walikwenda mbele zaidi na kumtafutia Harmonize pete ya uchumba amvishe Wolper huku wakiimba; ‘shemeji…shemeji…’ wakimuomba aolewe na jamaa huyo.

 

Akizungumza na Ijumaa Wikienda kuhusu tukio hilo, Wolper alisema kuwa hana mengi zaidi ya kushukuru kwani mabifu hayana maana.

 

Kwa upande wake, Harmonize alipozungumza na Ijumaa Wikienda alisema kuwa, Wolper ni mtu wake wa karibu na alifurahi kumuona akishiriki tena na Wasafi. Alipoulizwa juu ya mpenzi wake Sara atachukuliaje kitendo cha kugandana kimahaba na mpenzi wake huyo wa zamani, Harmonize alisema hawezi kumaindi kwani anaelewa kuwa wapo Mtwara kikazi.

STORI: MUSA MATEJA NA SHAMUMA AWADHI, MTWARA

Comments are closed.