The House of Favourite Newspapers

Wasanii wasisitizwa kujitambua, kujithamini na kujitangaza

Meza kuu ilivyokuwa wakati wa kongamano la kujadili tasnia ya uigizaji.

 

WASANII nchini wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kujijenga uwezo, kujithamini na kujitangaza iwapo wanataka kuiinua tasnia ya sanaa hiyo nchini.

 

Wito huo ulitolewa jana, Aprili 15, na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harisson Mwakyembe, katika kongamano la kujadili tasnia ya  uigizaji ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Suma JKT jijini Dar es Salaam.

 

Kongamano hilo liliandaliwa na Bodi ya Filamu nchini wakishirikiana na Chama cha Waigizaji ambalo liliwajumuisha waigizaji, watayarishaji na wadau wengine kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujitambua, kujithamini na kujitangaza.

 

Miongoni mwa wasanii waliohudhuria.

Miongoni mwa mambo aliyoyasisitiza Dkt. Mwakyembe ni  pamoja na kwamba wasanii kadhaa waliokuwa wakidai haki na malipo kwa kazi mbalimbali walizofanya hapo awali, tayari wamelipwa, akiwemo mwigizaji marehemu  Steven kanumba.

 

“Nimefurahi  kwamba kwa sasa mambo yanakuwa mazuri kwa kuwa jamaa wa State Entertainment wamelipa hela za marehemu Kanumba na ameshakabidhiwa mama yake na wamekubaliana watatengeneza filamu ambayo itaelezea maisha ya Kanumba,” alisema.

 

 

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harisson Mwakyembe (kulia) aliyekuwa mgeni rasmi.

 

Miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo walikuwa ni wasanii maarufu wakiwemo Wema Sepetu, thea, Davina Dino na wengine.

 

Akizungumza katika tukio hilo, Wema ambaye amekuwa akikumbwa na dhoruba ya kufungiwa mara kwa mara kufanya sanaa kutokana na vitendo vya kwenda kinyume na tasnia hiyo na maadili ya kitaifa, alisema marafiki zake ndiyo waliomfikisha alipo sasa.

 

“Marafiki ambao hawakupi kitu cha ziada na  ambao wao kila siku wanakunyonya tu, hutaendelea hata siku moja.  Kwa hiyo haya yote ni kutokana na marafiki ambao nilikuwa nao, na sasa nimejifunza kutokana na yanayonikuta,”alisema Wema.

 

 

Dkt. Mwakyembe akitoa ujumbe.

 

Katika kongamano hilo mafundisho mbalimbali yalitolewa ikiwa ni pamoja na mwigizaji kukuza, kulinda na kutangaza chapa (brand) yake, thamani ya uigizaji na umuhimu wa weledi katika kazi ya uigizaji.

 

Pamoja na hayo pia palisisitizwa mwigizaji kujikita katika kutoa filamu bora, kujipenda na kujithamini, kujikita katika ujasiriamali na nidhamu ya fedha, umuhimu wa mikataba na makubaliano kisheria, nafasi ya maisha ya kiroho na kufahamu umuhimu wa mitandao ya kijamii katika kukuza soko la waigizaji.

Na: NEEMA ADRIAN

Comments are closed.