WASTARA NATAMANI KUJIUAAN!

BINADAMU anaweza kuandamwa na matatizo kibao kiasi cha kufikia hatua ya kukufuru lakini hatutakiwi kuwa hivyo bali tunapopata mitihani tushukuru na kumuomba Mungu azidi kutulinda na shari!

 

Hivyo ndivyo anavyoweza kushauriwa msanii maarufu wa filamu Bongo, Wastara Juma ambaye hivi karibuni amepata janga lingine kubwa kiasi cha kufikia hatua ya kukata tamaa ya kuishi na kusema anatamani kujiua, Risasi Jumamosi lina habari yake ya kusikitisha.

 

Wastara ambaye amekuwa akisumbuliwa na tatizo la mguu wake wa kulia kwa muda mrefu baada ya kukatwa, bado amekuwa akipambana kujikimu kimaisha kupitia filamu lakini juzikati watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwake, Sinza-Kwa Remmy jijini Dar na kumuibia vifaa vyote vya ‘production’ pamoja na vitu vingine.

 

Taarifa ambazo zilitua kwenye meza ya Mhariri wa Risasi Jumamosi ilieleza kuwa, Wastara alifanyiwa umafia huo na watu wasiojulikana ambapo siku ya tukio saa 9 usiku walivamia na kuiba vifaa hivyo vya pruduction na baadhi ya kazi za filamu zilizokuwa zimekamilika.

 

“Jamani hivi mna taarifa za Wastara kuibiwa? Wamemvania pale Sinza anapoishi sasa hivi na kumuibia vifaa vyake vya production, hapa ninapoongea na wewe ana hali mbali sana, mtafuteni huenda akawaambia kilichotokea maana ishu iko polisi,” alisema mtoa habari huyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini.

WASTARA ATAFUTWA

Katika kupata undani wa tukio hilo, mwandishi wetu alimtafuta Wastara na kufanikiwa kumpata ambapo alifunguka juu ya majanga yaliyomkuta huku akisema kuwa, imefika wakati anatamani asiwepo duniani.

 

“Napita kwenye wakati mgumu sana jamani, kila likitoka hili, linaingia lingine, natamani hata nijiue. Ni kweli juzi nimeibiwa vifaa vyangu ninavyotumia kuzalishia filamu na vipindi vya TV, vifaa vina thamani kama ya milioni tisa hivi.

 

“Sielewi naanzia wapi, hapa nilipo nina kazi za watu ambazo zilikuwa kwenye ‘external’, nililetewa kwa ajili ya kuwafanyia kazi, wamechukua, kuna vipindi vya TV ambavyo nilikuwa nikivifanya kwa sasa sijui nitarekodi vipi tena, nimechanganyikiwa, natamani niondoke kwenye mgongo wa ardhi,” aliongea kwa uchungu Wastara.

 

NI MAJAMBAZI AU?

Akiendelea kusimulia, Wastara anasema kuwa, anahisi watu waliomfanyia umafia huo walikuwa na nia ya kumuua kwa sababu walipochukua kila kitu, hawakuondoka haraka wakidhani atatoka ili wammalize lakini Mungu akawa amemuokoa.

“Muda walionivamia pale nyumbani, baada ya muda mfupi ndugu yangu ambaye naishi naye akatoka nje, wakamvamia na kumkaba, nadhani walijua ni mimi. Walipoona wamemmaliza nguvu wakamuacha na kutimka zao,” anasema Wastara.

 

AHISI NI MCHONGO

Wastara anadai kuwa anahisi ni mchongo kutoka kwa watu wake wa karibu kwani majambazi hao hawakuvunja mlango na sebuleni kwake alikuwa amelala kijana mmoja lakini naye anadai hakusikia chochote.

 

“Kiukweli nahisi ni mchongo kwani kijana wangu aliyekuwa amelala sebuleni anadai hakusikia lakini mimi nahisi hata yeye anaweza kuhusika, haiwezekani ulale sebuleni halafu watu waingie usisikie chochote. “Mlinzi naye ambaye ni Mmasai eti hakusikia anadai alikwenda upande mwingine kukagua mazingira, kuna mchezo hapa,” alidai Wastara.

MSALA UKO POLISI

Kufuatia tukio hilo, Wastara alisema kuwa alilazimika kwenda kutoa taarifa polisi katika kituo cha Kijitonyama ‘Mabatini’ akiamini kupitia jeshi hilo wahusika wanaweza kupatikana na mali zake zikarudishwa.

 

“Ishu iko polisi, washukiwa wawili ambao ni mlinzi na kijana mmoja ambaye ananisaidia kazi zangu walikamatwa na kuwekwa ndani kwa siku nne. Yaani kikubwa nipate hata kamera yangu ya kazi maana nafikiria tena mambo ya kukodi kamera, sijui itakuwaje,” anasema msanii huyo.

 

ATOA OMBI

Wastara ameomba yoyote atakayeona kuna vifaa vya ‘production’ vinauzwa kuchunguza kama vina risiti na kama kutakuwa na uwezekano hata yeye kufahamishwa ikiwa ni sehemu ya kumsaidia. “Kwa yoyote atakayeona kuna kifaa cha production kinauzwa akakitilia shaka naomba anifahamishe huenda inaweza kunisaidia,” alimaliza Wastara.

 

TUJIKUMBUSHE

Wastara amekuwa akiandamwa na matatizo mbalimbali ambapo ukiacha lile la kukatwa mguu, amepata ajali kadhaa zilizomnusisha na kifo huku pia akiandamwa na misukosuko mbalimbali katika maisha yake ya kindoa.

Licha ya mitihani mizito ambayo amekuwa akiipata, bado Wastara amekuwa akiendelea kupambana ili aweze kujikimu kimaisha na amekuwa akiwaomba Watanzania wenzake waendelee kumuombea kwa Mungu ili amlinde na shari.

 

STORI: Hamida Hassan, RISASI JUMAMOSI

Toa comment