The House of Favourite Newspapers

WATOTO WANAOZUIA MVUA KUNYESHA

Image result for microcephaly baby in kenya

KWA zaidi ya muongo mmoja baadhi ya familia katika kaunti ya Kilifi nchini Kenya wamekuwa wakijifungua watoto wenye hali isio ya kawaida. Katika hali hiyo inayojulikana kama microcephaly ubongo wa mtoto haukui kama unavyohitajika kawaida,  hivyo kusababisha hali ya mtoto kuwa na kichwa kidogo ikilinganishwa na watoto wengine wa umri wao.

Hata hivyo, katika vijiji hivyo vya mashambani, jamii imekuwa ikiwatelekeza watoto wenye hali hiyo na sasa wamekuwa wakichukuliwa kama watu wenye laana na wanaosababisha majanga. Kulingana na wakazi wa vijiji hivyo, watoto wenye aina hiyo ya ulemavu wanaaminika kuzuia mvua kunyesha na hivyo kudaiwa kuwa chanzo cha baa la njaa katika vijiji maskini katika maeneo ya Bamba na Ganze.microcephaly

Hivyo, familia ambazo huwazaa watoto kama hawa hutakiwa kuwaua ama hata kulazimika kuhama vijiji hivyo ili kukwepa shutuma kutoka kwa wakazi wenzao. Familia moja kama hiyo ni ile ya mzee Ngumbao ambaye anasema kuwa alilazimishwa kuondoka nyumbani kwao huko Ganze na kuhamia katika mji wa Mtwapa uliopo kaskazini mwa mji wa Mombasa baada ya mkewe kujifungua mtoto mwenye ulemavu huo.

”Nililazimishwa kuondoka kijijini kwa sababu hakuna mtu aliyetaka kujihusisha na mtoto huyu. Hata wazazi wangu walikuwa wakiniambia nimuue ama hata kumtupa msituni,” anasema.

Ngumbao ambaye ni baba ya watoto watatu waliozaliwa bila ulemavu huo, anasema kuwa ametafuta msaada kutoka kwa baadhi ya madaktari kuhusu hali hiyo bila mafanikio yoyote. Hata hivyo, mtoto huyo Lela ambaye ana miaka 14  akiwa na umbo la mtoto wa miaka minne, amepata mahali anapopaita nyumbani katika shule maalum ya Sahajanad ambapo amejiunga na mamia ya watoto walio na ulemavu.

microcephaly

Kwake Leah, Shajanand ni shule ambayo anaweza kuchanganyika na watoto wenye ulemavu kama wake na kuweza kuishi bila kuhisi kwamba anabaguliwa na mtu yeyote yule. Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo Patrick Mzungu, watu wanaamini kwamba watoto hawa wanaleta bahati mbaya si tu kwa familia bali pia kwa jamii. Anasema kuwa baadhi ya watoto hao wamekuwa wakitumika katika matambiko kuwatakakasa wazee waliofariki na magonjwa ya zinaa.

Katika shule ya Sahajanand watoto hao wanaweza kutabasamu, wana udugu maalum na inaonyesha lengo lao la kutaka kuishi mbali na jamii ambayo imewakataa. Wengi ya watoto hao huletwa katika shule hiyo na wazazi ambao wanahofia maisha yao ama hata kuokolewa na utawala wa maeneo hayo. Katika jamii ambayo inaamini tamaduni zilizopitwa na wakati na ushirikina, watoto hawa hawana fursa ya kuishi nje ya kuta ndefu za shule hii.microcephaly

”Kuna mtoto ambaye tulimuokoa katika eneo la Baringo baada ya mvulana huyo kuangaziwa na vyombo vya habari kwamba alikuwa amefungwa kamba katika msitu ili afariki. Tulienda na vyombo vya habari kumuokoa mtoto huyo na sasa yuko hapa na ameimarika” anasema Mzungu.

Microcephaly ni nini?

Ugonjwa huo wa kichwa kidogo unahusishwa sana na Virusi vya Zika. Mnamo mwaka 2016 virusi vya Zika vilitangazwa kuwa janga la dharura ambalo limezua wasiwasi kimataifa. Zika ilitajwa kuwa ugonjwa hatari katika kiwango kimoja na ugonjwa wa ebola.

Lakini kile kinachowashangaza wengi ni idadi kubwa ya watu walio na ulemavu huo katika eneo hilo la mashambani la pwani ya Kenya. Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanaamini kwamba visa vya watu wa uhusiano wa karibu kujamiana huenda ndicho chanzo cha ongezeko la watoto wanaozaliwa na Microcephaly.  Lakini kulingana na daktari Ahmed Kalebi hali ni tofauti katika kaunti ya Kilifi.microcephaly

”Kuna data zinayoonyesha kwamba viwango vya microcephaly katika kaunti ya Kilifi iko juu ikilinganishwa na maeneno mengine duniani na hata Kenya, na baadhi ya tafiti zinasema kuwa huenda ugonjwa huo ukahusishwa na ugonjwa wa pepopunda. Sidhani iwapo tumefanya utafiti wa kutosha, lakini wakati kulipokuwa na mlipuko wa Zika kuna data inayoonyesha kwamba watu wa pwani ya Kenya wana viwango vya juu zaidi vya watu wenye kinga dhidi ya Zika’,’ anaeleza Daktari Ahmed Kalebi.

Wakati huohuo jukumu kuu la mwalimu mkuu Patrick Mzungu sasa ni kuhakikisha kuwa jamii yake inaelimishwa kuhusu hali hiyo, na pengine kuwashawishi kwamba huu ni ugonjwa kama mwengine wowote ule.

”Watoto hawa wana haki ya kuishi, hatukuenda kwa Mungu kumuuliza tuzaliwe na vichwa vidogo, hata wazazi hawakumuuuliza Mungu kuwapatia watoto wenye microcephaly, kwa hivyo tafadhilini sana hawa ni binadamu na ulemavu huu ni kama mwengine wowote ule tunaoishi nao,” anasema.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa kuna sababu nyingi za ugonjwa wa kichwa kidogo, hata hivyo chanzo chake hakitambuliki

Comments are closed.