The House of Favourite Newspapers

Watoto Wenye Ulemavu Wanastahili Kuoneshwa Utu na Kuthaminiwa

0

 

Ulemavu ni hali ya kuwa na hitilafu ya kudumu mwilini au akilini, inayomzuia mtu kutekeleza shughuli Fulani katika maisha yake tofauti na watu wengine. Lakini watu wenye ulemavu wakiwekewa mazingira rafiki kulingana na hitilafu zao wanaweza kutimiza majukumu yao kama mtu asiye na ulemavu na hata zaidi.

Katika hafla ya siku ya mtoto wa Afrika iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Chamazi na iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na watu wenye ulemavu la Androse Disability Organization Tanzania [ADOT], chini ya Mkurugenzi na Mwanzilishi wake Rosemary Choma, lilipata nafasi ya kuzungumza na watoto wenye ulemavu katika shule ya msingi Chamazi pamoja na Msufini.

Katika hotuba yao watoto hao wenye ulemavu waliishukuru serikali kwa hatua kubwa ya kuwasaidia watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu kwani sasa hata mtu mwenye ulemavu anaweza kupata elimu tofauti na hapo awali, lakini wameelezea changamoto ambazo wanapitia na kuiomba serikali, jamii pamoja na mashirika mbalimbali kuwasaidia ili waweze kupata elimu bora.

Changamoto hizo ni kama upungufu wa vyumba vya madarasa ambao unawafanya washindwe kupata elimu bora, miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu darasani pamoja na vyooni, ukosekanaji wa baiskeli zawanafunzi wenye ulemavu, hali inayowafanya wazazi kuwabeba watoto wao mpaka shuleni na maeneo mengine kila siku,huduma hafifu za matibabu kwani wengi wao hawana bima za afya, hali inayopelekea kina mama kupata tabu ya matibabu kwaajili ya watoto wao kwani wengi wao wametelekezwa na baba zao, vifaa vya michezo, upungufu wa walimu, uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Mbali na changamoto hizo ambazo watoto waliziorodhesha kwenye risala yao lakini watoto hao waliweza kuwasilisha changamoto nyingine kwa njia ya maigizo ambapo pia waliomba kuwepo na gari la kuwasaidia wakati wanakwenda shule na walitamani kuwepo na shule za bweni kwaajili ya wanafunzi wenye ulemavu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ADOT linaloshughulika na watu wenye ulemavu, Rosemary Choma, ambaye ndiye muandaaji wa hafla hiyo alipata wasaa wa kuzungumza na watoto hao wenye ulemavu huku akishukuru shirika la Tanzania Human Rights Defenders Coalition,kwa mchango mkubwa wa kufanikisha siku hiyo. Aliwataka wazazi na watoto wenye ulemavua kutokukata tamaa, kwenye kila jambo ambalo mtu asiye na ulemavu anaweza kufanya na wao pia wanaweza kufanya, na kuongeza kua watu wenye ulemavu wanamahitaji tofauti tofauti hivyo hawapaswi wakae kwenye kundi moja kimahitaji.

Ameeleza kua wao kama shirika lisilo la kiserikali na lisiloingiza faida, wamejipanga kusaidia katika changamoto ambazo zinawakumba watu wenye ulemavu kwani hata yeye amepitia changamoto hizo na anazifahamu, lakini kama shirika kwa kua bado ni changa na haliingizi faida yoyote hivyo wanapitia changamoto za kifedha, mkurugenzi amewaomba mashirika mbalimbali pamoja na wadhamini kuungana nao ili waweze kutekeleza majukumu ya kusaidia walemavu nchini.

Mkurugenzi pia ameeleza changamoto ambayo aliwahi kupitia yeye kama mlemavu wa miguu, ni wakati akiwa anasoma alishindwa kufaulu vizuri somo la kemia kwa vitendo kwani alikua akitumia magongo huku akitakiwa kuchanganya kemikali maabara hali ambayo ilikua ngumu kwake na kumfanya ashindwe kutimiza ndoto zake.

Hali hiyo japo ilimshtua na kumhuzunisha lakini haikumfanya kuendelea kukaa na kuomboleza bali alipata ari mpya ya kuangalia fursa nyingine, na sasa ameanzisha shirika lisilo la kiserikali kwa lengo la kupaza sauti ya utu, haki pamoja na maendeleo endelevu. ‘’ADOT itatibu na kuokoa roho nyingi sio tu kwa watu wenye ulemavu bali hata kwa watu wasio na ulemavu’’ Alisema Mkurugenzi huyo.

Alimalizia kwa kusisitiza kua shirika bado linaendelea kutafuta wahisani mbalimbali ili kuweza kusaidia walemavu, pia jamii iwajali watoto wenye ulemavu , wazazi wawe mstari wa mbele kwenye kuonyesha upendo kwa watoto na sio kuiachia serikali na vituo visivyo vya kiserikali kwani takwimu zinaonyesha watoto hao wenye ulemavu wanapitia unyanyasaji wa kijinsia, utelekezwaji, vipigo na hata kufanyishwa kazi ngumu jambo ambalo sio sawa.

‘’Watoto wenye ulemavu wanahitaji kutendewa utu kama ilivyo kwa mtoto asiye na ulemavu, ana haki ya kupendwa, kuwa na marafiki, kuishi, kupata elimu, kushirikishwa katika kufanya maamuzi, hawapaswi kufichwa ndani moyo wa mtu mwenye ulemavu hauna ulemavu’’.

Leave A Reply