The House of Favourite Newspapers

Watu 500 Wauwawa Kwenye Shambulizi La Hospitali Gaza

0

Zaidi ya watu 500 wameripotiwa kuuawa usiku wa Jumanne kwenye shambulizi ambalo limetokea hospitalini Ahli Arab katika Ukanda wa Gaza.

Wizara ya afya ya Hamas imedai shambulizi la angani la Israel ndilo limesababisha maafa hayo.
Lakini jeshi la Israel limekana kuhusika na kusema roketi ya Wanamgambo wa Kiislamu huko Gaza ndiyo imepiga hospitali.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ametangaza siku tatu za maombelezo baada ya mashambulizi hayo, kwa mujibu wa mamlaka za ukanda huo.

Kulingana na Israel, intelijensia ya jeshi lake imebaini kuwa roketi iliyofyatuliwa vibaya na wanamgambo wa Gaza ndiyo ilishambulia hospitali ya Ahli Arab.

Kupitia taarifa, msemaji wa jeshi la Israel amedai kuwa tathmini ya mifumo ya operesheni ya jeshi lao inaonyesha kuwa msururu wa makombora ulirushwa na magaidi huko Gaza. Amesema makombora hayo yalipita karibu na hospitali ya Al Ahli wakati iliposhambuliwa.

“Intelijensia tulizonazo kutoka vyanzo mbalimbali, zinaonesha wanamgambo wenye misimamo mikali ya Kiislamu, ndio wanawajibika kutokana na roketi iliyofeli na kupiga hospitali.”

“Kinachoendelea sasa ni mauaji ya kimbari. Tunaitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia haraka kuzuwia mauaji haya ya maangamizi. Ukimya haukubaliki,” ilisema taarifa iliyotolewa na Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) kinachoongozwa na Abbas.

Abbas na PLO walipoteza udhibiti wa Ukanda wa Gaza kwa kundi la Hamas baada ya uchaguzi wa 2006 uliofuatiwa na mapambano makali ya kuwania madaraka.

Haya yanajiri wakati rais wa Marekani Joe Biden akitarajiwa kuizuru Israel Jumatano, siku moja baada ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Tel Aviv.

Leave A Reply