The House of Favourite Newspapers

WAZAZI, WALEZI KULINDA WATOTO DHIDI YA UKATILI

Stori: Neema Adrian, Dar

Wazazi na walezi nchini wamekumbushwa kuwa na malezi chanya kwa watoto ili kukabiliana na ukatili unaoendelea dhidi yao.

Akizungumza na Gazeti la Ijumaa, mwenyekiti wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Thrive for Community Elevation (TCE), Rahim Ndambo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya malezi chanya katika Hoteli ya Serena jijini Dar alisema kuwa lengo ni kutatua tatizo la unyanyasaji dhidi ya watoto.

Alisema kuwa wameamua kukutana na wadau mbalimbali ili kuona ni namna gani wanaongeza nguvu na kushirikiana na Serikali katika kumaliza vitendo vya unyanyasaji. “Lengo ni kuwakumbusha wazazi kujenga ukaribu na watoto, kwani kwani unyanyasaji bado unaonekana kukithiri hapa nchini.

“Hii ni kulingana na ripoti ya mwaka 2017/2018 ya Jeshi la Polisi na Kituo cha Sheria za Haki za Binadamu (LHRC) ambayo imeanisha matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto uliongezeka kutoka matukio 4,728 hadi kufikia 6,376,” alisema Ndambo. Mwenyekiti wa Hakielimu, Richard Mabala ambaye alisoma hotuba kwa niaba ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM) ambaye ni mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Salma Kikwete alisema ni vyema tukaendelea kushirikiana kwa pamoja ili kumaliza tatizo hili.

“Ni vyema tukaendelea kushirikiana kwa pamoja ili kumaliza tatizo hili, unyanyasaji katika jamii bado upo, hivyo wazazi na walezi ni vyema wakaongeza suala la malezi kwa watoto wao,” alisema.

Comments are closed.