The House of Favourite Newspapers

Waziri Dk. Ndumbaro Awaagiza Wasanii Kujiunga Na Mfuko Wa Hifadhi Ya Jamii Ili Waje ‘Kukokotoa’ Mafao

0
Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro akizungumza na wasanii kwenye mkutano huo.

Dar es Salaam 6 Machi 2024: Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro amewaagiza wasanii nchini kujiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya kuwasaidia pindi wanapohitaji kustaafu au wanapopatwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kifo.

Waziri Dk. Ndumbaro alisema hayo jana Jumanne alipokuwa akizungumza na wasanii wa filamu na muziki kwenye kikao kilichofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar alipokuwa akiwasikiliza changamoto zao.

Katika kikao hicho Waziri Dk. Ndumbaro aliambatana na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini, Dk. Kiagho Kilonzo na Katibu Mtendaji wa Basata, Dk. Kedmon Mapana ambao nao walihusika kuyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi yale yaliyohitajika kufanyiwa kazi.

Baadhi ya wasanii kwenye mkutano huo kutoka kushoto, Khadija Kopa, Siza Mazongera wa Segere na Shoro Mwamba mwenye kofia nyekundu wakimsikiliza waziri kiumakini.

Wengi kati ya wasanii waliosimama na kuelezea changamoto zao walianza na kuzisifu Bodi ya Filamu na Basata kwa jinsi zilivyoweza kufanya nao kazi kiukaribu ikiwemo kuwaunganisha na wasanii wa kimataifa waliofika hapa nchini na kubadilishana nao mawazo hata hivyo wasanii hao walihitaji uboreshwaji zaidi wa tasnia hiyo.

Msanii wa Bongo Muvi, Mahsein Awadh maarufu kama Dokta Cheni kwa upande wake aliisifia Bodi ya Filamu kwa jinsi inavyoshirikiana kiukaribu na wasanii lakini aliiomba bodi hiyo kuwatafutia wasanii masomo ya nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza ujuzi wao na si kutegemea kuigiza kwa kipaji tu. Alisema kwa mtindo huo hawawezi kukua kisanii.

Mjomba akiwa makini kwenye mkutano huo.

Dokta Cheni ameeleza jinsi wapenzi wa filamu hapa nchini kila kukicha wanavyozidi kuzishabikia filamu za nje kutokana na ubora wake  na kusema hiyo inatokana na uwekezaji mkubwa wa kielimu na vifaa vinavyotumika kwenye kurekodia tofauti na wao ambao wanatumia vifaa duni na awana maboresho ya ujuzi ujuzi na kutegemea vipaji na ujanjaujanja.

Kwa upande wake Mfalme wa Taarab, Mzee Yusuf aliposimama alisema kwakuwa sanaa ni ajira kama ilivyo kauli mbiu ya sanaa hapa nchini ‘Sanaa Ni Ajira’ basi ifikie nao wasanii wawekewe mazingira ya kuwawezesha kiuchumi pindi wanapoamua kustaafu au kupatwa na changamoto kubwa ikiwemo kuugua au kifo wao au familia zao wapate pakushika na si kugeuka ombaomba na kudhalilika na familia zao.

Msanii wa Bongo Muvi, Loveness katika mkutano huo.

Hayo na mengine mengi yalijibiwa papohapo na Waziri Dk. Ndumbaro ambapo aliwaagiza Dk. Kilonzo na Dk. Mapana kuyafanyia kazi haraka ili watakapokuatana tena yote yawe yameshafanyiwa kazi huku suala la mafao Dk. Ndumbaro aliagiza ufanywe utaratibu wa wasanii hao kutafutiwa mfuko wa hifadhi ya jamii kwa ajili ya  kujiwekea akiba ambayo itawaokoa wao au familia zao endapo itatokea msanii kutaka kustaafu au maradhi, kifo na mengineyo.

HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS WA GPL

Leave A Reply