The House of Favourite Newspapers

MASAUNI AIOMBA PUMA KUSAIDIA UTOLEWAJI ELIMU YA USALAMA BARABARANI 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akimpa zawadi mmoja wa Wanafunzi wa shule ya msingi Bunge jijini Dar,mara baada kujibu vizuri swali lililohusu mambo ya usalama barabarani.
Mmoja wa watoa mafunzo ya Usalama barabarani kwa Wanafunzi wa shule za msingi chini ya Ufadhili wa kampuni ya Puma Energy Tanzania, Neema Swai kutoka taasisi ya AMEND akionesha moja ya mchoro ulioshinda kwenye shindano la Wachoraji kuhusu Usalama barabarani mwaka 2018.
Mwanafunzi Shule ya Msingi Bunge jijini Dar, Omari akifafanua kuhusu namna ya matumizi sahihi kwa watembea kwa miguu mbele ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchi ( wa tatu kulia ) Mhandisi Hamad Masauni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania,Dominic Dhannah akizungumza leo jijini Dar wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usalama barabarani.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akizungumza mbele ya wageni waalikwa. 
Mhandisi Hamad Masauni akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania akiwa na baadhi ya wanafunzi ambao ni Mabalozi wa shule ya msingi Bunge jijini Dar.

 

MAFUNZO ya elimu ya usalama barabarani yanayotolewa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy Tanzania kwa wanafunzi wa shule za msingi mbalimbali nchini yamemfurahisha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi, Hamadi Masauni ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa kampuni hiyo kuongeza wigo wa kutoa elimu hiyo.

 

 

Akizungumza leo Machi 18,2019 jijini Dar es Saalam wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya usalama barabarani kwa mwaka huu ambayo yamekuwa na kawaida ya kwenda sambamba na mashindano ya wanafunzi kuchora picha zinazozungumzia mambo ya usalama, Mhandisi Masauni amesema Puma imeamua kufanya kitu cha kuigwa na kampuni nyingine na wanastahili pongezi.

 

 

Amesema Serikali inafarijika na kazi inayofanywa na Kampuni ya Puma kwa kurudisha faida inayopatikana kwa jamii ikiwamo kutoa mafunzo muhimu ya usalama barabarani.

 

Amesema elimu ni suala la kipaumbele kwa jamii na mkakati wa wao Wizara ya Mambo ya Ndani na Serikali kwa ujumla ni kupunguza ajali za barabarani na Puma inafanyakazi hii kwa karibu na mnamo Machi 30, mwaka huu kutakuwa na kongamano la wiki ya usalama barabarani.

 

 

“Serikali tunatambua kazi nzuri ambayo inafanywa na Puma Energy Tanzania katika kutoa elimu hii inayohusu usalama barabarani. Ni jukumu letu na wananchi kwa ujumla kuunga mkono jitihada hizi.,” alisema Masauni.

 

Akifafanua zaidi Mhandisi Masauni amesema kitendo cha Puma kuwa na programu hiyo kinaonesha namna ambavyo wanakataa ajali za barabarani kwa vitendo na kwamba wanafunzi ambao wanapata elimu hiyo anauhakika watakuwa mabalozi wazuri wa kuelezea kwa usahihi mtembea kwa miguu anatakiwa kufanya nini akiwa barabarani.

 

 

“Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama Barabarani wana program nyingi za kusaidia kutoa mafunzo kwa shule zote zilipo kwenye mazingira hatarishi na zisizo kwenye mazingira hayo pia. Programu hizo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali za kifedha. Ninaomba kutumia fursa hii kuomba uongozi wa Puma kukisaidia Kikosi cha Usalama Barabarani kuzifikia shule zote nchini kwa kupitia askati walioko kwenye maeneo yote nchini,”amesema.

 

 

Pia amemuagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuanza mchakato wa kuandaa andiko la kutoa mafunzo kwa shule zote nchini na kuliwasilisha kwa (Puma) ili waone namna yambavyo wanaweza kusaidia kuokoa kizazi  cha kesho,” alisema Masauni.

 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania Dominic Dhanah amefafanua kuwa mafunzo hayo yanakwenda sambamba pia kwa wanafunzi waliowahi kufundishwa.

 

Amesema madhumuni ya kuwahusisha wanafunzi wa shule za msingi ni kutokana na imani yao kwamba, watoto hao wanakabiliwa na hatari za ajali za barabarani na kuhitaji mafunzo ya usalama barabarani ili kuepukana na ajali.

 

“Usalama barabarani ni kipaumbele namba moja katika Kampuni ya Mafuta Puma na tumeamua kuwafundisha watoto wadogo kwani tunafahamu hatari za barabarani wanazokabiliana nazo. Kampuni ya Puma inafanya biashara ya mafuta katika nchi 49 duniani na kwa Afrika tupo katika nchi 19. Mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi yalianza mwaka 2013 hapa Tanzania na mpaka sasa shule 75 zimenufaika na mafunzo haya wakati wanafunzi 80,000 wamepata mafunzo haya,”amesema.

 

Ameongeza kuwa “Tumefanya utafiti na kugundua kuwa shule tulizoendesha mafunzo haya , ajali kwa wanafunzi zimepungua na hivyo basi kwa mwaka 2019 mafunzo haya yataendeshwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar,” alisema Dhanah.

 

 

Comments are closed.