WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesifu juhudi za Benki ya NMB kwenye kuunganisha jamii kupitia huduma bora za kibenki, matukio ya michezo na hata misaada mbalimbali nia ikiwa kuona jamii ya kitanzania inashiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa Taifa.
Alitoa kauli hiyo juzi jijini Dodoma kwenye Bonanza la michezo lililowashirikisha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wafanyakazi wa Benki ya NMB.
Akizungumzia kuhusu utendaji wa benki ya NMB, amesema imekuwa ikishirikiana na Serikali kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kufungua akaunti na kujiwekea akiba.
“Benki ya NMB ni benki pekee iliyomudu kufungua matawi hadi maeneo ya vijijini, hivyo kurahisishha upatikanaji wa huduma kwa watumishi na wananchi waishio maeneo hayo.”
Amesema ni muhimu kwa watumishi kushiriki katika michezo mbalimbali kwa kuwa inaimarisha afya pamoja na kudumisha mshikamano.
Michezo iliyochezwa katika bonanza hilo ni mpira wa miguu ambapo timu ya Bunge ilishinda baada ya kuifunga timu ya benki ya NMB magoli matano kwa matatu.
Kwa upande wa mchezo wa mpira wa pete timu ya Bunge iliibuka na ushindi baada ya kuifunga timu ya NMB magoli 25 kwa 18, huku katika mchezo wa mpira wa kikapu timu ya NMB ilishinda baada ya kuifunga Bunge vikapu 54 kwa 52.
Katika mchezo wa kuvuta kamba timu ya Wabunge Wanawake na Wanaume waliibuka na ushindi baada ya kuzishinda timu za NMB.
Comments are closed.