The House of Favourite Newspapers

WAZIRI WA UJENZI, MAWASILIANO NA USAFIRISHAJI ZANZIBAR AIPONGEZA TTCL

Mhandisi wa Mitambo ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Aman Kichere (kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Mhe. Dk. Sira Ubwa Mamboya (katikati) namna mitambo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano inavyofanya kazi. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Bw. Waziri Kindamba akishuhudia. 
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Mhe. Dk. Sira Ubwa Mamboya (kushoto) akizungumza mara baada ya ziara yake kutembelea  Miundombinu na Mitambo ya Mawasiliano inayosimamiwa na TTCL Corporation.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation Bw. Waziri Kindamba (mwenye kipaza sauti) akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Dk. Sira Ubwa Mamboya (kushoto) alipotembelea miundombinu na Mitambo ya Mawasiliano inayosimamiwa na TTCL Corporation.
…Waziri Kindamba (kushoto)  akifafanua jambo kwa Waziri Dk. Sira Ubwa Mamboya (kulia mbele).
… Dk.  Mamboya (mbele) akitembelea miundombinu na mitambo ya mawasiliano inayosimamiwa na TTCL Corporation. 

 

WAZIRI wa AUjenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Sira Ubwa Mamboya, amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Shirika la Mawasiliano Tanzania ( TTCL Corporation) katika kutoa huduma bora za Mawasiliano na usimamizi wa Miundombinu ya Kimkakati ya Mawasiliano Nchini.

 

 

Mhe Waziri Dkt. Sira Ubwa Mamboya, ametoa pongezi hizo Jijini Dar Es Salaam mara baada ya ziara yake katika Shirika la Mawasiliano Tanzania, kutembelea Miundombinu na Mitambo ya Mawasiliano inayosimamiwa na TTCL Corporation.

 

Katika salamu zake, Mhe Waziri amepongeza utendaji wa TTCL mpya ambayo inafanya juhudi kubwa za kuliimarisha Shirika na huduma zake na kuonesha kufurahishwa na utaratibu wa Shirika hilo kutoa ajira kwa kuzingatia pande zote za Muungano hali inayoimarisha udugu na uhusiano mwema.

 

 

Akizungumza katika salamu za kumkaribisha Mhe. Waziri, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation Bw Waziri Kindamba amewashukuru viongozi Wakuu wa SMZ kwa uongozi wao thabiti unaodumisha Muungano na kustawisha ushirikiano unaoiwezesha TTCL Corporation kutimiza vyema majukumu yake katika Ofisi zake zote Tanzania Visiwani ambapo inaihudumia Serikali, Taasisi za Umma na Sekta binafsi.

 

 

“Tunapopata ugeni kama huu, tunafarijika sana kwani kupitia tukio hili, uhusiano mwema wa kindugu baina ya pande mbili za Muungano unaimarishwa, Aidha, tunabadilishana ujuzi na uzoefu pamoja na kujenga mtazamo wa pamoja wa namna bora zaidi ya kuwahudumia Wananchi wetu” amesema Kindamba.

 

 

Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation lilizaliwa  Februari 01, 2018, kwa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2017. Kuundwa upya kwa Shirika hili la TTCL Corporation ni matokeo ya kukamilika kwa mchakato wa kutunga sheria uliopitia katika hatua zake zote ikiwemo kuridhiwa na Bunge na hatimaye kupata idhini ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 28, 2017.

 

 

Huduma za mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zinazosimamiwa na kuendeshwa na TTCL zimeiwezesha Tanzania kuwa Nchi ya kupigiwa mfano katika Ukanda wa kiuchumi wa Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na kuwa na mfumo mzuri zaidi kukusanya kodi kwa kutumia mfumo maalumu wa kielektroniki wa Serikali ujulikanao kama GePG.

Comments are closed.