BAADA YA WIMBO WAKE KUPIGWA MUSCAT… BABA DEE, WANAYE KIMEELEWEKA

DAR ES SALAAM: KIMEELEWEKA! Ndivyo unavyoweza kusema, baada kuwepo kwa kutoelewana kwa muda mrefu, hatimaye moshi mweupe umeonekana baada ya baba wa msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Abdul Juma kupatana na mwanaye huyo pamoja na dada yake Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’.

 

WIMBO WACHANGIA

Kupatana kwa baba Diamond na wanaye hao ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawapatani kumechagizwa zaidi na ishu ya wimbo ambao mshua huyo ameshirikishwa kutikisa Muscat nchini Oman ambako Diamond na familia yake walikwenda kufanya shoo inayofahamika kwa jina la Wasafi Festival.

ILIVYOKUWA MUSCAT

Wakiwa nchini humo, Diamond aliyeambatana na mama yake mzazi Sanura Kassim ‘Bi Sandra’ na dada yake Esma Khan, walishuhudia DJ wa Diamond, Rommy Jones akiuanzisha wimbo huo alioshirikishwa baba Diamond uitwao Dudu la Yuyu kabla ya shoo ya Wasafi kuanza.

 

SHANGWE KAMA LOTE

Rommy alionesha makeke ya kuimba wimbo huo uliotrendi baada ya kuachiwa hivi karibuni na ndipo mamia ya watu waliofurika katika shoo hiyo walipolipuka kwa shangwe baada ya kuutambulisha kwamba umeimbwa na baba yake Diamond.

 

WANANZENGO SASA

Kufuatia kipande cha video ambacho kilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki iliyopita, mashabiki wengi walioonekana kuguswa na baba Diamond, walimshauri amshtaki maana ameutumia wimbo wake bila idhini yake. “Baba Diamond tuko pamoja na wewe, mshtaki tu kwa nini wimbo wako autumie kule?” aliandika mdau mmoja mtandaoni huku akiungwa mkono na wenzake kibao.

IJUMAA LAMSAKA BABA MONDI

Ili kuweza kujua baba Diamond amezipokeaje taarifa hizo za wimbo wake kutumika huko Muscat na kama bado ana bifu na wanaye, Ijumaa Wikienda lilimtafuta mshua huyo ambapo alipopatikana alifunguka mengi. Kwanza alisema anamshukuru Mungu wimbo huo umemfanya aelewane na wanaye sababu wameonesha kumuunga mkono na hata yeye hana tena kinyongo nao.

 

“Nimeona hiyo video huko mitandaoni ikisambaa, ambapo wimbo nilioimba unapigwa huko Muscat Oman, nimefurahi kuona mtoto wangu ananikubali na kuusapoti sana wimbo wangu, mpaka amefikia hatua ya kuuimba mitandaoni hii inamaanisha kwamba wimbo ni mzuri na wameukubali,” alisema baba Diamond.

 

KIMEELEWEKA

Alipoulizwa maneno ya mashabiki wake yaliyomtaka amchukulie hatua za kisheria kwa kuutumia wimbo huo bila idhini yake, baba Mondi alisema haoni sababu ya kufanya hivyo sababu wao tayari wameshamaliza tofauti.

 

“Nimefurahi, sitaki wanilipe kabisa eti kwa sababu wameupafomu jukwaani, Diamond ni kijana wangu kwa hiyo hata akitaka aupofomu sehemu nyingine mimi sina tatizo kabisa, sitaki anipe pesa yoyote ile ila kama atajisikia kunisaidia hata kidogo basi atanitafuta na atanisaidia maana anajua nina tatizo langu la miguu linalonisumbua muda mrefu,” alisema mzee huyo.

 

SAPRAIZI YA MAMA MONDI

Kuonesha kwamba sasa hivi hakuna tena bifu, baba Diamond alimweleza mwanahabari wetu jinsi alivyopigiwa simu hivi karibuni kama sapraizi na mama Diamond ambaye ana muda mrefu hakuwahi kuwasiliana naye.

 

“Diamond na Queen Darleen nimeshukuru nao nimeona wanasapoti wimbo lakini mama Nasibu ndio amenisapraizi hivi karibuni alinipigia simu akiwa mwenye furaha tele akaniambia wimbo mzuri na najua kuimba basi tuliongea vizuri naamini kila kitu kitakwenda vizuri kuanzia sasa,” alisema baba Diamond.

WAMEMALIZA BIFU JUMLA?

Licha ya kuwa bado hawajakutana, baba Diamond alipoulizwa kama bifu lao limeisha jumla, alisema yeye ameshawasamehe wanaye hao na kwa mazungumzo yake na mama Diamond, anaamini wakirudi kutoka Muscat basi watakutana uso kwa uso na kugonga glasi pamoja.

 

“Tuko sawa kwa sasa, ninachowaomba tu mimi kwa sasa wanisaidie hili tatizo langu la miguu basi maana kwa kweli linanitesa,” alisema baba Mondi.

 

TUJIKUMBUSHE

Kwa muda mrefu, Diamond na Queen Darleen walikuwa kwenye bifu zito na mzazi wao huyo kiasi ambacho mzazi huyo alifikia hatua ya kuwalaani huku Queen Darleen akiongoza kwa kumchana maneno mabaya mzazi wake huyo. Kwa kipindi chote hicho, hakuna yeyote kati yao aliyekuwa anamposti au kumzungumzia mazuri mwenzake zaidi ya kuombeana mabaya.


Loading...

Toa comment