The House of Favourite Newspapers

WEMA AMKA, JIPANGUSE NA UKIMBIE!

Wema Abraham Sepetu,

TANGU ametwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Abraham Sepetu, hajawahi kuchuja. Nyota yake ilianza kung’ara tangu aliposhiriki mashindano ya Kitongoji cha Dar Indian Ocean na baadaye Miss Kinondoni.  

 

Hadi leo kila anachogusa Wema anatusua. Jamii inamkubali na anao mashabiki wengi wanaomfuata katika kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii. Hakuna ubishi kuwa  kati ya warembo wote waliopata kuchukua ulimbwende wa Tanzania, Wema ndiye anayeongoza kutunza ustaa wake.

 

Kismati cha Wema kinachobebwa na haiba yake, kujiamini na mvuto wa kipekee alionao, kilizidi kuchanja mbuga alipotia maguu katika ulimwengu wa sinema za Kibongo. Marehemu Steven Kanumba, ndiye aliyekuwa chanzo cha Wema kuingia kwenye filamu, baada ya kumchezesha sinema yake ya kwanza iitwayo A Point of No Return. Hakuna aliyeamini alichokiona katika sinema ile.

 

Wema alionyesha uwezo wa hali ya juu. Baada ya pale zilifuata filamu nyingi, akiendelea kuonyesha ukomavu wake. Mfano mzuri ni 14 Days, Red Valentine, Dj Ben na White Maria. Wema amekuwa akikubalika katika kila anachokifanya kisanii na kijamii. Kuna wakati alikuwa akiendesha kipindi chake cha matukio yanayomtokea kila siku; kipindi alichokiita In My Shoes, mashabiki walikuwa wakisubiri kila wiki kuona kitakachoendelea.

 

Mbali na yeye ni msanii wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Jide’ pekee ndiye aliyepata kuwa na kipindi binafsi cha televisheni alichokipa jina la Diary ya Lady Jaydee, kikakubalika. Pamoja na hayo, ni kama Wema anaonekana kutoitambua thamani yake. Anaishi maisha asiyostahili kabisa kutokana na jina na heshima aliyonayo kwenye jamii.

 

Kofia mbili alizonazo – Miss Tanzania na mwigizaji, zinampa nafasi ya kutengeneza maisha bora, lakini hafanyi hivyo. Kuna wakati alianza kufurukuta taratibu, lakini ghafla akarudi chini. Sote tunakumbuka Wema wakati akifungua kampuni yake iitwayo Endless Fame ambayo ilijipambanua kujihusisha na utayarishaji filamu na wasanii wa Bongo Fleva, ambapo wa kwanza kabisa alikuwa ni Mirror.

 

Wema ambaye anaweza kujaza ukumbi peke yake kwa tukio la uzinduzi wa filamu pekee, kwanini anashindwa kutumia nafasi hiyo kujitajirisha? Tunakumbuka wakati akizindua sinema yake ya Superstar. Miongoni mwa wasanii nyota waliohudhuria ni pamoja na Omotola Jalade kutoka Nigeria.

 

TUJIKUMBUSHE

Huko nyuma Wema aliwahi kuzindua lipstick yake, bidhaa aliyoipa jina la Kiss By Wema Sepetu. Ni bidhaa iliyopendwa na mashabiki wengi. Je, bidhaa hiyo imeishia wapi?

 

Kadhalika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Wema alijaribu bahati yake kwenye ulingo wa siasa baada ya kujitosa kugombea Ubunge wa Viti Malaamu kupitia UVCCM Mkoa wa Singida. Pamoja na kwamba kura hazikutosha, lakini ushindani aliouonyesha ulikuwa mkubwa ambao unapaswa kumpa picha kwamba, akiamua kwa dhati kupambana, anaweza kwa kuwa anakubalika.

MAISHA YA MAIGIZO

Ni vema sasa Wema akaachana na maisha ya maigizo. Staili hiyo siyo nzuri, kwani huwashusha wasanii badala ya kuwapandisha.

 

Huko nyuma mara kadhaa Wema amefanya maigizo; kuna wakati alidai amenunua nyumba na aliita waandishi wa habari ambao walifanya naye mahojiano na kupiga picha za video na mnato zikarushwa kwenye vyombo vya habari. Lakini baada ya miezi kadhaa ukweli ukabainika kwamba haikuwa nyumba yake, bali alipanga. Kuna sababu gani ya kudanganya maisha? Wema anapaswa kuangalia maisha yake na kubadilika, maana njia ya mafanikio yake bado ipo wazi.

 

Kuna wakati alikuwa akidaiwa kuwa na urafiki na wanaume tata hadi kufikia hatua ya kuishi nao nyumbani kwake. Hayo anapaswa kuachana nayo, afungue ukurasa mpya.

 

AJIFUNZE KWA JOKATE

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo anaweza kuwa mfano mzuri kwa Wema. Akimwangalia huyo anaweza kujifunza kitu na kuanza upya, maana muda bado unaruhusu. Ni miss mwenzake, ambaye alikuwa nyuma yake katika nafasi ya pili kwenye Fainali za Miss Tanzania mwaka 2006. Ana miradi kadhaa ambayo anaisimamia na inafanya vizuri. Mbali na miradi, Jokate ana mfuko wa kusaidia watoto wa kike. Lakini kubwa zaidi, ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, nafasi anayoitendea haki.

WEMA KIMBIA

Kwa jinsi Wema alivyo na nyota, alipaswa awe mbali sana kimafanikio. Muda hausubiri, ukipita imetoka. Juzi Jumatano, alifungua duka lake la nguo za watoto lililopo Kinondoni alilolipa jina la Little Sweetheart. Kama nilivyosema hapo juu, ipo miradi kadhaa ya Wema ambayo haijulikani ilipoishia, hapa anatakiwa kukaza.

 

Wema anatakiwa kuhamishia nguvu zake katika duka lake hilo, lakini pia aangalie namna ya kuanzisha na kuendeleza miradi mingine itakayokuza kipato chake. Ukweli ni kwamba amechelewa sana kusimamisha miradi yake, lakini anatakiwa kujifunza kwa yaliyopita na sasa aamke upya, kwani mafanikio yake yapo jirani. Kukubalika ni mtaji wa kipekee. Wema alitambue hilo.

Na Joseph Shaluwa

Comments are closed.