The House of Favourite Newspapers

WINNIE MANDELA; MWANA MKE WA CHUMA

 

Nelson Mandela na Aliyekuwa mkewe, Winnie.

JUMAPILI iliyopita, wakati watu mbalimbali duniani wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka, katika familia ya mpambanaji, mhamasishaji na mwandishi wa vitabu Winnie Mandela, kulitawala majonzi tele baada ya kifo cha mwanamama huyo.

Winnie akiwa na miaka 81, alifariki katika Hospitali iitwayo Netcare Milapark, huko Johannesburg, kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi tangu uanze mwaka huu.

 

Lakini pia alikuwa ni mke wa Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, na ni miongoni mwa wanawake wa chuma duniani ambaye hatuwezi kuacha kumzungumzia hasa kwenye makala haya ambayo ni mahususi kwa wanawake, kwani siku ya leo mwanamake unayesoma makala haya unaweza kujifunza mengi!

Kuanzia uvumilivu kwenye masuala ya ndoa, pia namna alivyoyafanya maisha yake kuwa na maana kutokana na kutumia kipajia chake cha uandishi wa vitabu lakini pia kutokana na kazi za kijamii alizofanya mpaka anakumbukwa baada ya kifo chake.

Wengi wanaweza kujiuliza kuwa Winnie pia alikuwa miongoni mwa wanawake matajiri duniani? Jibu ni kwamba inawezekana kabisa hakuwa kwenye listi hiyo, na hapa nitakukumbusha kitu kimoja, mafanikio kwenye maisha hayamaanishi pesa tu. Ni zaidi ya pesa na kila mmoja anaweza kuyaelezea kwa namna yake.

Ndiyo maana leo unaweza kumuona Bill Gate, mmoja wa watu waliofanikiwa zaidi duniani kwenye suala zima la pesa akipaa kutoka Marekani mpaka Afrika kwa ajili ya kula maharage na watoto wa shule au yatima!

Kwa akili ya kawaida unaweza kujiuliza anatafuta nini kwa kufanya kwake hivyo. Ukweli ni kwamba anayafanya maisha yake kuwa na maana kwa watu wengine.

 

Kwa hiyo kwa wewe mwanamke wa chuma unayesoma makala haya kwa kile ambacho unakifanya, kwanza mtangulize Mungu, kisha jipe moyo na fanya kazi kwa bidii. Hata kama usipoona mafanikio ya fedha haraka kwa kile unachokifanya kuna watu ‘utawainspire.’

Lakini pia kuna msemo hapa kwetu Afrika, unasema ukifanya kile unachokiamini na kukipenda kwa asilimia mia moja hata kama majibu usipoyaona leo, basi utayaona kesho. Lakini pia ni bora ya yule mtu anayetembea taratibu kuliko aliyesimama kabisa. Kwa hiyo usichoke kupambana.

 

Tukirudi kwa Winnie, ambaye toka mwaka 2009 mpaka mauti yanampata alikuwa ni miongoni mwa wabunge wa taifa hilo kupitia Chama cha ANC (African National Congress), lakini pia anahesabika na kuheshimiwa kama mama wa Taifa la Afrika Kusini.

Kwa pamoja, yeye na Nelson Mandela walipambana kuhakikisha taifa hilo linakuwa huru kutoka kwa Makaburu lakini pia wakati Mandela amefungwa kifungo cha maisha jela aliendelea kusimama imara na kuwahamasisha wapigania uhuru kupambana mpaka haki ikapatikana na baada ya miaka 27, mumewe akaachiwa.

Mandela, Winnie na Mwl. Nyerere.

Vitabu alivyoandika ni pamoja na 491 Days: Prisoner Number 1323/69 cha mwaka 2013, Une Part de mon ame, Part Of My Soul Went With Him alichokitoa kipindi Mandela yupo jela.

Hata hivyo kutokana na mwanamama huyu aliyezaa watoto wawili na Mandela ambao ni Zenani na Zindziwa, kuyafanya maisha yake kuwa na maana katika jamii, mwaka 2011, mastaa wa filamu duniani Terrence Howard na Wendy Crewson, wakiongozwa na dairekata Darrell Roodt, waliandaa filamu ya maisha yake.

 

Mbali na filamu hiyo, mwaka 1984, Winnie alizawadiwa Tuzo ya Freedom Of The City Of Aberdeen na mwaka 1988, akapewa nyingine ya United Nations Prize In The Field Of Human.

Huyo ndiye Winnie Mandela. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi lakini akiwa katika mapumziko ya milele wazaliwe kina Winnie Mandela wengine.

Makala: Boniphace Ngumije

Comments are closed.