The House of Favourite Newspapers

Yanga: Hamtaamini Kitakachotokea Kwao

Kikosi cha timu ya Yanga.

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, amesema wengi hawataamini kitakachotokea kwani wamepanga kushangaza mashabiki wao kwa matokeo mazuri watakayopata katika mchezo wao wa marudiano dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

 

Nsajigwa ametoa kauli hiyo baada ya mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga ilifungwa mabao 2-1.

 

Timu hizo zinarudiana Machi 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa uliopo Gaborone, Botswana ambapo moja kati ya viingilio vyake ni Pula 40, sawa na Sh 9,240.

 

Ili iweze kusonga mbele, Yanga inatakiwa kushinda kuanzia uwiano wa mabao 2-0 ambapo itakuwa imeingia moja kwa moja katika hatua ya makundi, kinyume na hapo itacheza mtoano na timu za Kombe la Shirikisho ili kufuzu hatua ya makundi.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Nsajigwa alisema benchi lao la ufundi chini ya Kocha Mkuu Mzambia, George Lwandamina wameona udhaifu wa wapinzani na wamepanga kuufanyia kazi ili kuhakikisha wanapata ushindi ugenini.

 

Nsajigwa alisema, Rollers ni wepesi na wanafungika kirahisi baada ya kuwaona katika mchezo uliopita na kikubwa kilichosababisha washindwe kupata ushindi nyumbani ni baadhi ya wachezaji kushindwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake.

 

“Rollers siyo wazuri wa kufikia hatua ya kukata tamaa ya kufanya vizuri katika mchezo ujao wa marudiano, nikuhakikishie kuwa kama wachezaji wetu watacheza kwa kufuata maelekezo yetu vizuri, niamini tunakwenda kuwatoa nyumbani kwao.

 

“Wanayanga wanatakiwa kuendelea kutupa sapoti ili katika mechi hiyo ya marudiano tupate ushindi mzuri utakaotupeleka katika makundi, mashabiki hawataamini kitakachotokea.

 

“Katika mchezo uliopita, tulishindwa kuwadhibiti katika kiungo na tukawaacha wakatawala na kusababisha kupiga pasi nyingi, kitu ambacho tumekiona na tunakifanyia kazi kisijirudie,” alisema Nsajigwa.

 

Akizungumzia mechi hiyo, beki wa pembeni Hassan Kessy alisema: “Kama wao walitufunga hapa nyumbani kwetu kwa nini sisi tushindwe kuwafunga kwao? Tunakwenda kuwafunga kwao kwani ni timu ya kawaida, kikubwa tunaomba sapoti ya mashabiki.”

 

Kwa upande wake, Gadiel Michael alisema: “Tulipoteza mechi ya hapa nyumbani kutokana na makosa madogo, tunafanya marekebisho tukawafunge kwao kwani baadhi ya majeruhi wamerudi.”

 

Kiungo Pappy Kabamba Tshishimbi yeye alisema: “Soka ni mchezo wa makosa ambayo tuliyafanya na wenzetu wakayatumia kutufunga, hivyo hatutaki kurudia makosa hayo badala yake tutapambana kwa nguvu ili tushinde.”

STORI: WILBERT MOLANDI | CHAMPIONI JUMAMOSI

Comments are closed.