Yanga Hii Inahitaji Huruma Maalum, Vinginevyo Aibu
UNAWEZA kudhani kama ni mchezo wa kuigiza kuona klabu kubwa inaingia kwenye mapito magumu ya kiuchumi, Kiutawala na kiuchezaji na mara nyingi jambo hili linapotokea basi utaona taswira nzima ya uendeshaji wa klabu inayumba na kupoteza muelekeo.
Yanga na Simba ndizo klabu zinazotajwa kuwa kubwa hapa nchini lakini usifikiri kwamba ukubwa unaozungumzwa unalenga moja kwa moja kwenye maendeleo yanayotakiwa kuwepo kwenye klabu yenye hadhi ya ukubwa la hasha! hapa unatajwa ukubwa wa kuzaliwa.
Yanga imezaliwa au kuanzishwa mwaka 1935 na Simba ikaanzishwa mwaka mmoja baadae yaani mwaka 1936, hapa utakubaliana nami kwamba hizi ndizo klabu kongwe kuliko zote zilizopo katika nchi yetu.
Klabu hizi kubwa zimekuwa na mfanano wa kiuendeshaji kwakuwa zote zinatumia mfumo wa wanachama katika maamuzi makubwa yanayohusu klabu,hivyo mara nyingi utaona jambo linapojitokeza Yanga linaweza kujitokeza pia upande wa Simba,na ndiyo sababu klabu hizi zimepachikwa jina la Kurwa na Doto.
Hebu sasa turudi kwenye lengo kuu la makala haya,klabu ya Yanga kwa sasa inaonekana kupoteza muelekeo kwa kiasi kikubwa hasa kutokana na kukabiliwa na mvurugano wa kiuendeshaji unaosababishwa na makundi yaliyojitengeneza ndani ya klabu hiyo yenye wanachama na mashabiki wengi kuliko klabu nyingine yeyote hapa nchini.
Kuwepo kwa makundi yanayohusisha wanachama pamoja na viongozi waliochaguliwa na kuteuliwa ni kasumba iliyojengwa kwa miaka mingi kiasi cha kufanya klabu kushindwa kujipambanua kimataifa na badala yake huishia kutamba tu hapa nyumbani licha ya kuwa na wachezaji wa kigeni wanaowasajili kwa gharama ya kufuru.
Baada ya kuukosa ubingwa wa msimu uliomalizika ambao umechukuliwa na majirani zao Simba,Yanga ilianza kubomoka taratibu kuanzia kwenye kamati ya usajili ambayo ilijisahau na kujiona kuwa yenyewe ndiyo yenye jukumu la mwisho katika maamuzi, kana kwamba hawajui kuwa ipo kamati ya utendaji juu yao iliyokabidhiwa majukumu ya uratibu na utekelezaji kwa matakwa ya kikatiba.
Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, kamati ya usajili kazi yake kubwa ni kusikiliza na kupokea mapendekezo au maagizo ya benchi la ufundi kuhusu kuongeza au kuwaondoa wachezaji fulani kikosini na baada ya hapo Kamati inapeleka mapendekezo hayo kwenye kamati ya utendaji kwa utekelezaji.
Hivi karibuni Abbas Tarimba ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Yanga,alikabidhiwa uongozi wa kamati ya usajili kwa lengo la kuisuka upya klabu hiyo iliyobomoka lakini cha kushangaza likaibuka kundi linalotajwa kukereketwa na maendeleo ya klabu likapinga uamuzi huo naye kuamua kujiuzulu.
Uchunguzi makini wa makala haya umebaini kwamba kundi hilo lililochanganyika na watu waliomo kwenye kamati hiyo hapo kabla limepinga uamuzi wa mkutano mkuu kuikabidhi kamati mikononi mwa Tarimba,kwa kile kinachotajwa kuwa huenda akaziba mirija waliyokuwa wakiitumia kupitishia 10% za usajili, kutokana na msimamo madhubuti alionao.
Kwa hali ilivyo sasa nadhani Yanga inahitaji ‘huruma maalum’ ili kuiokoa katika mapito magumu inayopitia wakati huu ambao inahitaji kufanya usajili wenye kiwango na siyo kusajili wachezaji magarasa walioshindwa kuwika kwenye klabu walizotoka.
Niwape ushauri wa bure nyie wanayanga,njia pekee ya kuirudisha klabu yenu kwenye mstari ni kuitisha mkutano mkuu wa dharura na kufanya maamuzi magumu katika safu nzima ya uongozi kwa kuwaondoa wasiofaa na kuwabakiza wenye uchungu wa kweli wa matatizo wa klabu bila kumuonea mtu.
Na baada ya hapo hakikisheni kwa pamoja mnavunja makundi yaliyopo na kuwa pamoja, mkizungumza lugha moja na hatimaye kuilinda klabu isivamiwe tena na viongozi mizigo kwa kuwa tayari mtakuwa mmesha wabaini,kinyume na hapo mtapata tabu sana.
NA OMARY KATANGA | CHAMPIONI JUMAMOSI
Comments are closed.