The House of Favourite Newspapers

Yanga SC: Msituchukulie Poa

Wachezaji wa timu ya Yanga wakiendelea na mazoezi.

KUELEKEA mchezo wake dhidi ya Azam FC leo Jumamosi, Yanga imesema ina kikosi imara cha kupata ushindi na wale wote wanaoiona timu yao ni dhaifu, wasiwachukuliwe poa kwani wamejipanga kushinda.

 

Yanga ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, itakuwa mgeni wa Azam iliyopo nafasi ya pili, katika mchezo wa ligi hiyo leo kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar.

 

Katika ligi kuu, Yanga na Azam zimekutana mara 18, hivyo mchezo wa leo ni wa 19 huku Yanga ikiwa mbele kwa kushinda mechi sita na Azam ikishinda mara tano na wametoka sare mara saba. Yanga imefunga mabao 24 huku ikiruhusu mabao 22 wakati Azam ina mabao 22 na ikiwa imefungwa mabao 24.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, amesema: “Ni mchezo muhimu na ni mgumu kwa kila upande, kila timu inahitaji matokeo ili kutengeneza nafasi nzuri kwenye ligi.

 

“Kucheza Chamazi kwetu si ugenini kwani nayo ni Dar es Salaam, hatuna shaka na hali ya hewa, tumecheza hapo mara kadhaa na tunafahamu mazingira yote ya uwanja huo. “Tunawaheshimu Azam, wamekuwa na matokeo mazuri msimu huu, Yanga pia tuna uwezo wa kupata matokeo mazuri uwanja wowote.”

Katika ligi kuu, Yanga kwenye michezo mitatu iliyopita imeshinda mmoja dhidi ya Ruvu Shooting bao 1-0, ikatoka suluhu na Mwadui FC lakini huko nyuma ilifungwa mabao 2-0 na Mbao FC, hivyo kuzua hofu kwa mashabiki wake. “Watu wasituchukulie poa, wanapaswa kuiheshimu Yanga, wanaposema Azam ipo vizuri kuliko Yanga, na mimi nitawaambia Yanga ipo vizuri kuliko Azam, huu ni mpira wa miguu, kila timu inahitaji kuheshimiwa,” alisema Ten.

 

Kuhusu suala la Azam kutokuwa na imani na mwamuzi wa leo, Israel Nkongo, Ten amesema: “Wao wanakumbushia waamuzi wafuate sheria 17 za soka, sisi hatuwezi kusema kitu ila tunataka uamuzi wa haki.” Katika mchezo huo, Yanga itawakosa nyota wake saba wenye matatizo mbalimbali ambao ni Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Yohana Nkomola, Pato Ngonyani, Pius Buswita, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Donald Ngoma.

Katika mazoezi yao ya mwisho jana Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, nyota hao hawakufanya mazoezi wakati Kocha George Lwandamina akiwapa wachezaji wengine mbinu za kuikabili Azam. Lwandamina alionekana kuwa makini katika kuunda mifumo mitatu anayotegemea kuitumia leo dhidi ya Azam ambayo ni 4-42, 3-5-2 na 4-3-3, huku jukumu la ufungaji likiwa kwa Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu.

 

Wakati huohuo, mpaka jana Ijumaa, kibali cha Lwandamina kilikuwa kipo kwenye hatua za mwisho za kupatikana ili leo aweze kukaa kwenye benchi la timu hiyo baada ya kukosekana katika michezo miwili ya ligi iliyopita dhidi ya Mwadui na Ruvu Shooting. “Tumeshafanya taratibu zote kuhakikisha suala la kibali linakamilika kilichobaki ni upande wa serikali kukitoa, tuna imani leo (jana Ijumaa) mambo yatakuwa mazuri,” alisema Ten. Kwa upande wake, Azam kupitia kwa kocha wake msaidizi, Idd Cheche, amesema: “Tunataka kushinda ili tulinde heshima yetu ya kutopoteza mchezo nyumbani, tunafahamu hautakuwa mchezo rahisi ila tumejipanga kushinda.”

Na Omary Mdose na Musa Mateja

Comments are closed.