The House of Favourite Newspapers

Yanga VS Simba…Dakika 20 Kazi Kwisha

Kikosi cha timu ya Yanga.

JUMANNE jioni Kocha wa Yanga,Mwinyi Zahera na Wachezaji wake walikuwa wametulia hotelini wanacheki mechi ya Simba na Ahly iliyokuwa inapigwa Taifa. Baada ya ile gemu akawaambia wachezaji wake hawa jamaa Jumamosi tutawashindwa jamani… wachezaji wakamwambia tunaanzaje sasa!

 

Zahera amewaambia wachezaji waliopiga kambi kwenye hoteli ya Kingsway, Msamvu kwamba anataka ndani ya dakika 20 tu wawe wameshamaliza kiherehere cha Simba.

 

Jana mazoezini kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia Bigwa, kama ambavyo wanaonekana kwenye picha amewasisitiza wachezaji watulize mzuka mechi ya
Jumamosi ni yao kabisa, wala wasiwe na presha.

 

Kina Yondani wakamwambia wala usiwe na wasiwasi Kocha wale wetu kabisa. Zahera amewaambia wakishapata bao hilo ndipo waanze kupaka rangi. Kocha huyo anayeishi Ufaransa, amewaambia wachezaji kwamba Simba wataingia kwenye mchezo huo kwa papara na majivuno ya ushindi wa Ahly hivyo watawabana kirahisi.

Zahera ameliambia Spoti Xtra mjini hapa kwamba tayari amefanyia marekebisho ya kikosi chake kwa kuziboresha baadhi ya sehemu ikiwemo safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Heritier Makambo, Amissi Tambwe, Haruna Moshi Bobani na nahodha wake Ibrahim Ajibu.

 

“Nimeona mbinu wanazozitumia Simba katika mchezo wa Al Ahly kupitia televisheni, hivyo sina hofu nayo kikubwa hivi sasa ninakiboresha kikosi.

 

“Ninajua Simba wataingia uwanjani na papara baada ya kupata ushindi mechi na Al Ahly lakini hiyo hainipi hofu ninajua
wenyewe wataingia wakitaka ushindi, hivyo ninawatoe hofu Wanayanga kuwa, ushindi upo,” alisema Zahera.

RAPHAEL KARUDI

Kiungo mchezeshaji Raphael Daudi jana rasmi alianza mazoezi magumu na timu hiyo na atacheza Jumamosi. Raphael anarejea kwenye kikosi hicho akitoka kwenye majeraha ya misuli aliyoyapata wakati timu hiyo ilipocheza na Biashara United ya Mwanza katika mchezo wa ligi. Zahera alisema kuwa kurejea kwa kiungo huyo kutaimarisha kikosi katika kuelekea katika mchezo huo wa watani wa jadi. Zahera alisema, tofauti na kuimarisha kikosi chake, pia kutaongeza ushindani wa namba katika nafasi yake inayochezwa na Issa Mohammed ‘Banka’, Haruna Moshi ‘Boban’ na Pius Buswita.

YONDANI

Kelvin Yondani amesikia mbwembwe za Simba baada ya kuifunga Al Ahly juzi Jumanne akawaambia subiri Jumamosi tutaona pale Taifa.

Mchezaji huyo mkongwe aliyewahi kucheza Simba amewaambia kwamba; “Kwa jinsi ambavyo tunaelewana kwa sasa, sitarajii kuona Simba wakipata ushindi mbele yetu, zaidi mchezo utakuwa mgumu na wakupambana ila wao ndiyo wajipange zaidi kupoteza mbele yetu, maana kwa sasa sisi ni wa moto kupita maelezo,” alisema Yondani.

TAMBWE Zahera jana alimuondoa Amissi Tambwe mazoezini baada ya kujitonesha goti lakini akasisitiza kwamba atakuwa sawa kabla ya Jumamosi.

 

KAMBINI Katika kambi ya Yanga kuna ulinzi mkali wa walinzi wa kampuni binafsi ya Ulinzi pamoja na mlinzi wa kambi. Mazoezini pia hakuna anayeruhusiwa kuingia bila ruhusa maalum kutoka kwa uongozi.

WILBERT MOLANDI

Comments are closed.