The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaipita Simba Pointi 19, Matokeo Mechi za Jana Yapo Hapa

Kikosi cha timu ya Yanga.

KOCHA Mwinyi Zahera juzi aliwaambia mashabiki wa Yanga mjini Mwanza kwamba atavunja mwiko wa kufungwa na Mbao ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba. Wakamuangalia kama vile wanamuelewa lakini nyuso zao zikaonekana watu wenye hofu. Baada ya matokeo ya jana jioni wakamuelewa na wakalala raha mustarehe.

 

Yanga ilishinda mabao 2-1 na kufikisha pointi 61. Kabla ya mechi ya jana, Yanga ilipoteza mara zote mbili ilizocheza na Mbao kwenye uwanja huo, ya kwanza ikipigwa bao moja na iliyofuata ikalam bwa mbili.

Lakini jana Zahera akafuta historia hiyo na kuandika mpya. Kabla ya kupanda basi kuelekea uwanjani, Zahera aliwasimamisha wachezaji pembeni nje ya hoteli akawaambia ambaye anaamini wanakwenda kushinda apande kwenye gari na ambaye haamini abaki, wote wakapanda na basi likaondoka wakiwa na morali ya hali ya juu. Hiyo inamaanisha kwamba Yanga iliyocheza michezo 25 imeizidi Simba inayokula viporo kwa pointi 19.

 

Simba ina pointi 42 ikiwa kwenye nafasi ya tatu. Ingawa hawakuwa na mashambulizi mengi hatari kipindi cha kwanza, Mbao walipata bao la kuongoza dakika ya 45 kupitia kwa Ndaki Robert, Yanga wakaenda vyumbani vichwa chini jambo ambalo lilimlazimu Zahera kuwasisitiza wachezaji wake warudi uwanjani ngwe ya pili wakishambulia kwa nguvu na kutumia krosi zenye macho. Straika Mkongomani, Heritier Makambon dakika ya 49 aliisawazishia Yanga kwa kichwa akiunganisha krosi ya raia mwenzie, Pappy Tshishimbi. Dakika ya 68, Amissi Tambwe alifunga bao la ushindi kwa njia ya penalti baada ya Erick Muliro kuunawa mpira uliopigwa na Kelvin Yondani.

 

Awali kabla Tambwe ambaye amefikisha mabao saba hajapiga penalti, Ibrahim Ajibu alikimbia kumkumbatia Yondani akimpongeza kwa kusababisha penalti hiyo na kuwathibitishia mashabiki kwamba hawana bifu. Mchezo huo ulionekana kuwa hamsini kwa hamsini muda mwingi, ingawa Yanga walionekana kutumia zaidi

uzoefu huku Mbao wakikosa mshambuliaji wa mwisho.

 

Yanga wakati wanaingia vyumbani walikanyaga mstari wa katikati ya uwanja, huku mashabiki wa Mbao wakiingia na punda na wakiwa wameshikilia vitu mbalimbali mikononi vitendo vyote viwili vikiashiria ushirikina.

Baada ya mchezo huo, Zahera alisema; “Tuliporudi vyumbani niliwaambia wachezaji wangu wakumbuke tumekubaliana nini.

 

Niliwaambia kwamba hawa Mbao wametufunga lakini hawajafanya hatari yoyote, chakufanya turudi tuwashambulie kwa nguvu na kupiga krosi za haraka. “Na kweli wamefanya nilichowaagiza na mechi ikamalizika kirahisi,” alisema kocha huyo huku mashabiki wa Yanga wakiimba nyimbo za kuikejeli Simba kwamba iendelee na viporo vyao wao sasa ni mbele kwa mbele na kila mtu ashinde mechi zake.

MATOKEO MENGINE

MBEYA CITY 0 1 PRISONS

KMC 1 0 MTIBWA

NDANDA 2 0 SINGIDA

STAND 3 2 LIPULI

Comments are closed.