The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaizidi Ujanja Mbao Mwanza

YANGA imeizidi ujanja Mbao FC kwani licha ya kutanguliza watu wake wa kuweka mambo sawa, viongozi wa timu hiyo Tawi la Mwanza nao wameandaa mikakati ya kuwazima wapinzani wao.

Mbao kesho Jumapili itakuwa mwenyeji wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa. Msimu uliopita Yanga ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo uwanjani hapo.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu Mipango wa Tawi la Yanga Mwanza, Hashim Omar amesema wameandaa mikakati kabambe ya timu yao kushinda.

 

“Tunajua Mbao ni timu nzuri na inakuwa na uwezo mkubwa inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani lakini kuelekea mchezo wetu, hatutaruhusu kufungwa tena.

“Tumejipanga kuvunja mwiko wa kutowafunga Mbao kwenye uwanja wao wa nyumbani, tumejiwekea mikakati ambayo tunaamini Yanga inashinda pale,” alisema katibu huyo.

Omary akiwatoa hofu Mbao, alisema wao kama viongozi wanaamini katika sheria 17 hivyo hawajaandaa mkakati wa nje ya uwanja ili kushinda.

 

Wakati huohuo, Yanga katikati ya wiki hii ilitanguliza kundi la viongozi na wanachama wake jijini Mwanza kuhakikisha wanaweka mazingira sawa kabla ya mchezo wao dhidi ya Mbao.

Kikosi cha Yanga kilitarajiwa kuwasili Mwanza jana kwa ndege kutoka Dar es Salaam na kilifanya mazoezi ya mwisho juzi asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Johnson James, Mwanza

Comments are closed.