YANGA ni kama imejibu mashambulizi baada ya juzi usiku kumshusha mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Benin na Klabu ya Buffles du Borgou FC ya nchini huko, Marcelin Degnon Koukpo na jana usiku alitarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Vigogo wa Yanga wamemshusha mchezaji huyo ambaye inadaiwa kwamba ndiye mbadala wa Amissi Tambwe ambaye inaonekana maji yamezidi unga na huenda wakaachana nae kama ilivyokuwa kwa Donald Ngoma aliyetua Azam kwa Hans van Der Pluijm.
Tambwe alikuwa akiwakosha Yanga kutokana na uwezo wake wa kutupia hata kwa vichwa ambavyo Mbenin huyo amewaambia viongozi kwamba hiyo ni kazi ndogo kwake kwani amekuwa akiifanya maranyingi.
Marcelin alitua nchini juzi Alhamisi usiku akitokea kwao Benin kwa ajili ya kumalizana na Yanga akiwa kama mchezaji huru na kama mambo yamekwenda sawa jana huu utakuwa ndiyo usajili wa kwanza wa Kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera.
Mbenin huyo mwenye miaka 23, tofauti na uwezo wa kupiga vichwa, pia viongozi wa Yanga wanadai wameambiwa na kocha kwamba ana uwezo wa kupiga mashuti ya mita 20.
Yanga ambayo bado haijaimarika kiuchumi, inafanya maboresho katika safu ya ushambuliaji haswa kutokana na kuwepo kwa uwezekano wa Mzambia, Obrey Chirwa kuibukia Simba kuchukua nafasi ya Laudit Mavugo ambaye ameshaambiwa kwamba hana chake.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi imezipata, mshambuliaji huyo hadi anatua nchini alikuwa tayari ameshamalizana na viongozi wa Yanga na imebaki kutia dole gumba tu na kwenda Kenya kuungana na wenzake wanaoshiriki michuano ya SportPesa inayoanza kesho.
“Hadi anakuja hapa nchini mshambuliaji huyo viongozi walikuwa wamemalizana kila kitu ikiwemo dau la usajili na muda wa mkataba ambao yeye alifikia makubaliano mazuri ya kusaini.
“Hivyo, mshambuliaji huyo anasaini mkataba leo usiku (jana) na kesho (leo) asubuhi anatarajiwa kupanda ndege kwenda Kenya kujiunga na wenzake kwenye michuano ya SportPesa,” kilisema chanzo chetu.
Mwenyekiti wa Kamati Usajili wa Yanga, Hussein Nyika jana jioni hakupatikana kufafanua lakini Championi linajua kwamba mchezaji huyo ameletwa kwa ushirikiano na Kocha Mwinyi Kaheza.
Alhamisi iliyopita Nyika alisikika akisema wamepanga kufanya usajili mkubwa ambao utashangaza wengi na hawakurupuki kwenye mipango yao.
Comments are closed.