The House of Favourite Newspapers

Yanga Yapoteza Mamilioni ligi kuu

LICHA ya Klabu ya Yanga kuwa katika mchakato wa kusaka fedha kwa kufanya mchakato wa kutembeza bakuli kwa mashabiki wake, lakini imejikuta ikipoteza zaidi ya shilingi milioni 18 ‘kizembe’ kwa makosa ya nidhamu ya kukiuka taratibu za michezo ya kutoingia katika mlango rasmi.

 

Yanga ambayo ipo katika mchakato wa kusaka fedha za usajili, imejikuta ikipoteza kiasi hicho cha fedha katika mechi zake nne kwa makosa ya kutumia milango isiyo rasmi na kutoingia vyumbani jambo lililosababisha kupigwa faini katika mechi zote nne ikiwemo dhidi ya Coastal Union, Simba, KMC na Ndanda FC ya Mtwara.

 

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maarufu kama Kamati ya Saa 72, hadi sasa imeshaipiga faini Yanga mara nne katika mechi tofauti ikiwa ni zaidi ya Sh milioni 18 walizotakiwa kulipa ambapo wameyafanya makosa hayo bila ya kujali hali yao ya kiuchumi ndani ya klabu.

 

Aidha, mara ya pili Yanga ilijikuta ikipokea faini nyingine katika mchezo wa nambari 270 dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar, kwa kurudia kosa hilo Februari 16 la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi pamoja na kutoingia katika vyumba vya kubadilishia nguo, hivyo ikijikuta ikilambwa faini ya Sh milioni 6.

 

Katika mchezo mwingine dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa Taifa, Yanga ilijikuta ikipoteza Sh milioni 6 kwa mara nyingine kutokana na kupigwa faini kwa kosa lilelile la kuingia mlango usio rasmi katika mchezo huo pamoja na kutoingia vyumbani katika vyumba vya kubadilishia nguo.

 

Vilevile katika mchezo wa hivi karibuni dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona Aprili 4, Yanga ilirudia kosa hilo ikiwa ni mara ya nne kutokea katika msimu huu tangu ligi ianze.

 

Bodi ya Ligi imeamua kuitoza tena faini ya shilingi milioni 3 kwa kosa la kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi ikiwa ni pamoja na kutozwa shilingi laki tano kutokana na mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wakati wakirejea vyumbani, hivyo kusababisha wapoteze shilingi milioni 18.5.

 

Aidha, adhabu hizo za Yanga zimetolewa na bodi ya ligi kwa kuzingatia Kanuni ya 14 (49) ya ligi kuu toleo la mwaka 2018 kuhusu taratibu za michezo.

Comments are closed.