The House of Favourite Newspapers

Yanga Yashusha Kipa Mcongo

ACHANA na yule kipa wa TP Mazembe, Vumi Ley Matampi aliyeta­jwa anakuja Yanga, timu hiyo ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha usa­jili wa kipa mpya Mcongo anayetarajiwa kutua nchini leo.

 

Kipa huyo anatarajiwa kutua nchini kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo akichukua nafasi ya Mcam­eroon, Youth Rostand anayeta­jwa kuachwa katika usajili wa msimu huu.

 

Yanga hivi sasa ina makipa watatu pekee ambao ni Benno Kakolanya, Ramadhan Kabwili na Rostand mwenyewe ambaye alikuwa namba moja katika kikosi hicho.

 

Kwa mujibu wa taarifa am­bazo imezipata Championi Ju­matano, kutoka kwenye benchi la ufundi hiyo kipa huyo anaye­tarajiwa kutua nchini ambaye jina lake ni siri anatokea kwenye moja ya klabu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Congo.

Mtoa taarifa huyo alisema, kipa huyo anakuja Yanga baada ya Matampi kupata ofa nzuri nchini Saudi Arabia ambako alikwenda baada ya kushindwa­na naye katika dau la usajili.

 

Aliongeza kuwa, kipa huyo analetwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Zahera Mwinyi ambaye amepewa jukumu la kuleta kipa mwenye kiwango cha juu zaidi ya Ros­tand.

 

“Kocha ndiye aliyepend­ekeza asajiliwe kipa mwingine profesheno mwenye kiwango cha juu zaidi ya Rostand, hivyo basi kama uongozi tumeona tu­muachie yeye hilo apendekeze kipa anayeona anafaa kwake.

 

“Hivyo, kocha tayari yupo kwenye mazungumzo na kipa kutoka DR Congo anayecheza Ligi Daraja la Kwanza ambaye ni mzuri kwake anasema anafaa kuja kuichezea Yanga,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Zahera alisema: “Ni kweli kabisa timu ina tatizo la golikipa, hivyo ninahitaji kipa mwingine mzuri wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa zaidi ya Rostand.

“Nipo katika hatua za mwisho na kipa mmoja kutoka Congo ambaye jina lake nisingeweza kuliweka wazi kwa hivi sasa kama unavyofahamu usajili wetu tunaufanya kimyakimya na kama kila kitu kikikamilika basi nitaweka wazi.”

Comments are closed.