The House of Favourite Newspapers

Yanga Yatumia saa 72 Kupangua Hujuma

YANGA ni kama imefanikiwa kwa asilimia kubwa kukwepa hujuma za wapinzani wao, St Louis ya Shelisheli, baada ya kutuma viongozi wao nchini humo ambao wana siku tatu sawa na saa 72 tangu wakiwa huko kuhakikisha wanapata ushindi ugenini.

Timu hiyo, iliondoka nchini jana saa mbili kamili asubuhi tayari kwa ajili ya kurudiana na wapinzani wao hao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa keshokutwa Jumatano.

Msafara huo wa wachezaji wa Yanga uliondoka ukiwa na nyota wake 20 huku wakimbakisha mshambuliaji wao tegemeo Mzambia, Obrey Chirwa mwenye maumivu ya misuli.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mkuu wa msafara wa timu hiyo, Hussein Nyika ambaye ni Mwenyekiti wa Mashindano na Usajili ya timu hiyo, alisema kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukwepa hujuma za wapinzani wao baada ya kutanguliza viongozi huko watakaowapokea nchini humo.

Nyika alisema, viongozi hao wamewaandalia hoteli uzuri watakayofikia na uwanja wa kisasa ambao watafanyia mazoezi kabla ya mechi hiyo.

“Kama unavyojua mpira una mambo mengi ya ndani na nje ya uwanja, hivyo kama viongozi tumejitahidi kuanza nalo hili la nje ya uwanja kwa maana ya kuandaa hoteli nzuri itakayofikia timu na uwanja mzuri tutakaotumia kwa ajili ya mazoezi kwa siku mbili hizi.

“Kazi hiyo waliifanya jopo letu la viongozi ambao wapo huko kwa muda wa siku tatu kwa ajili ya kukwepa mipango hiyo ya nje ya uwanja kwa maana ya hujuma.

“Ninafurahia kuona wachezaji wetu wakiwa na morali ya hali ya juu katika kufanikisha ushindi huo katika mechi hiyo muhimu ambayo tunahitaji ushindi wa aina yoyote ili tusonge mbele katika mashindano hayo,” alisema Nyika.

“Kikosi kipo fiti na mchezo huo baada ya benchi letu la ufundi kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mechi yetu iliyopita dhidi ya Majimaji (Yanga ilishinda 4-1), hivyo tuna matumaini makubwa ya ushindi,” alimalizia Nyika.

Na Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.