The House of Favourite Newspapers

‘Yatapita’ Yamuweka Simorix The General Meza Moja na Diamond

0
Simon Masanja Simorix The General  (Jeneral).

Imekuwa ni kawaida kwa msanii Naseeb Abdul, ‘Diamond Platnumz’ kugawa fursa mbalimbali pindi anapoachia wimbo wake mpya ila hii utapita imekuwa tofauti.

Diamond Platnumz ndani ya mwaka huu tayari ameachia ngoma mbili zinazosumbua anga la muziki Afrika, Yatapita na Zuwena. Nyimbo hizo zenye asili kamili ya Bongo Fleva ndio ngoma pendwa kwa sasa.

Diamond Platnumz amefaulu kwa kiwango kikubwa kuwakusanya mashabiki wa enzi zile za Kamwambie na Mbagala, nyimbo zinazobeba simulizi ya vijana wengi wapambanaji wanavyoteswa na hali mbaya za uchumi kwenye sekta nzima ya mapenzi.

Maudhui hayo, ya wimbo Yatapita imekuwa ngoma pendwa ikichagizwa na ubunifu mkubwa wa kifilamu ulioonekana kwenye video kiasi cha kuibua maelfu ya vijana wanamuziki waliovutiwa kutengeneza remix za wimbo huo.

Diamond amezoea kuwapa fursa wasanii wachanga, wakati huu ameachia fursa mpya kwa wasanii wa aina zote za muziki kufanya remix ya wimbo, Yatapita na atakayemkosha yeye na jopo lake basi wataingia studio kurekodi wimbo mpya.

Ukisharekodi wimbo na Diamond basi tambua milango imeshakufungukia, Afrika imeshakujua na atafanya mchakato wa kukuweka karibu ili nawe utoboe kama ambavyo amesaidia wasanii wengine kupaa.

Miongoni mwa marapa wachache waliotumia vizuri fursa hiyo ni Simon Masanja maarufu kama Simorix General, rapa Mtanzania anayeishi nchini Australia ambaye tayari ameingia kwa miguu yote kwenye anga la Diamond Platnumz.

Simorix ambaye tayari amefanya ngoma nyingi na mastaa wa Tanzania, safari hii amefanikiwa kuwashika watu wa karibu na Diamond Platnumz punde baada ya kuachia remix yake ya Yatapita na kuonyesha utofauti mkubwa.

Muda mchache baada ya kuachia video ya wimbo Yatapita Remix, watu kama Baba Levo na wengineo katika mtandao wa Instagram walijikuta wakiachia jumbe za kufurahia aina ya maudhui aliyoyafanya Simorix kwenye ngoma hiyo.

Simorix mwenye swaga za kinyamwezi anapofanya rap zake, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuonyesha ubunifu ambao wasanii wengine wameshindwa kuonyesha kwenye shindano hilo ambalo sasa Diamond anapata shida kutafuta Top 10.

“Kuona watu wa karibu na Diamond Platnumz wameupokea vizuri wimbo wangu ni ushindi tosha, kilichobaki ni mapokeo ya mashabiki ili big mwenyewe aone kuna haja ya mimi na yeye kuingia studio kufanya ngoma,” amesema Simorix.

Akizungumzia Yatapita Challenge Accepted, Simorix The General, ametamba kwamba katika ngoma za wasanii wote walioingia kwenye shindano hilo yeye ndio amewekeza pesa nyingi ili kupata kitu bora kinachofanana na kile cha Diamond Platnumz.

“Nafikiri mimi ndio yule msanii ambaye Diamond Platnumz alikuwa anamsubiri kwenye challenge hii, nimekwenda mbele zaidi ya wasanii wengine kwenye rap yangu na uwekezaji, ukicheki video ilivyo kali utagundua jinsi ambavyo nimedhamilia kupata nafasi hii ya kufanya kazi na Diamond Platnumz, ” amesema Simorix.

 

Leave A Reply