The House of Favourite Newspapers

Yondani Amuweka Wazi Mrithi Wake Stars

BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, amefunguka kuwa anaamini beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto, ndiye ana uwezo wa kuziba nafasi yake iwapo ataamua kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

 

Yondani ametoa kauli hiyo kufuatia beki huyo kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (Chan) dhidi ya Sudan ambao Stars imefuzu kwa faida ya bao la ugenini.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Yondani alisema kuwa anaamini beki huyo ana uwezo mkubwa wa kuchukua mikoba yake ndani ya kikosi hicho kutokana na kucheza kwa utulivu mkubwa pamoja na kutumia akili ya kupambana na washambuliaji kama ilivyokuwa kwa upande wake.

 

“Binafsi naona yule Mwamnyeto anaweza kucheza kwenye nafasi yangu vizuri katika kikosi cha timu ya taifa, kwa sababu amekuwa akicheza kwa utulivu mkubwa na anajua vizuri kupambana na washambuliaji.

 

“Naamini atakuwa msaada maana uchezaji wake hautofautiani na mimi, mara kadhaa nimekuwa nikimpigia simu kumueleza hilo kwa sababu navutiwa na uchezaji wake na hata kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Chan dhidi ya Sudan ubora wake umeonekana,” alisema Yondani.

Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Comments are closed.