INAWEZEKANA hii ikawa ni zaidi ya mara ya 50 au hata ikifika mara 100 kwangu nitaona sawa tu kama somo likiendelea kutoeleweka kusema kuwa soka la sasa ni biashara, nitaendelea kurudia tu kwa kuwa kuna watu wanalijua hilo lakini wanafanya makusudi kuzuia kwa faida zao binafsi.
Wakati Yusuf Manji alipokuwa akianza mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu ya Yanga alikugusia pia juu ya umiliki wa klabu hiyo, kauli yake ilikuwa ni kama kisu kwa baadhi ya watu, wapo waliompinga kwa nguvu kubwa.
Mimi nilikuwa mmoja wa watu waliounga mkono mabadiliko ndani ya Yanga na niliwahi kuandika hapa kuwa lolote ambalo litafanyika kipindi hicho hasa kama l i t a h u s i s h a m a b a d i l i k o ya kimfumo lazima liwe na kasoro, hivyo i t a t e g e m e a wahusika watazitumia vipi hizo kasoro zao kufanya m a b o r e s h o ya kile wanachokitaka.
Yanga na Simba ni klabu kubwa na zenye nguvu kubwa ndani ya Tanzania, huwezi kusema unabadilisha mfumo wa uendeshaji kisha ndani ya muda mfupi kila kitu kinakaa sawa, hasa kwa kuwa kuna watu wanazitumia kuendesha maisha yao ya kila siku.
Manji ni mfanyabiashara nilieleza hata kwenye kolamu yangu hii kuwa hakuna mfanyabiashara ambaye anapenda kufanya kitu kwa hasara, hata kama ni tajiri mkubwa kiasi gani, hawezi kuwa anatoa tu fedha bila kuwa na mpangilio maalum wala bila kujua zitarudi vipi.
Alipokuwa akitoa misaada mingi ya kifedha nilijua ipo siku atataka irejee kwa njia anayoijua yeye, hata kama ilimchukua muda mrefu kusema au kuweka wazi kile alichokuwa nacho kichwani lakini huo ndiyo ukweli kuwa Manji alikuwa na nia nzuri ya Yanga.
Siku zote unapokuwa kwenye vita kutokea kutofautiana na wenzako au kumshambulia mwingine bahati mbaya ni mambo ya kawaida, Manji siyo malaika, alikuwa na makosa yake ya wazi na mengine ambayo hatuyajui, lakini vita aliyopigwa ilikuwa nzito na yawezekana ilimzidi nguvu ndiyo maana akaishia njiani.
Wanayanga wengi walikuwa wanajisifu kwa timu yao kutokuwa na njaa na shida za fedha ndogondogo, hilo ni kweli liliwezeshwa na Manji lakini wanatakiwa kukubali kuwa fedha hizo zilikuwa zikitoka katika njia ambayo siyo sahihi, kama wanaosimamia soka wangeamua kusimamia masuala ya matumizi ya fedha basi Yanga wangeingia kitanzini.
Katika soka kuna kitu kinaitwa ‘financial fair play’ yaani fedha za soka zitumike katika masuala ya soka, Yanga kwa asilimia kubwa chini ya Manji ilitumia fedha za mfukoni za bosi wao huyo na ndiyo maana walikuwa wababe, hivyo Manji alilijua hilo na ndiyo maana akasisitiza kuwa ni vema njia sahihi zikafuatwa.
Alitaka hilo kwa kuwa hakutaka kuendelea kutoa fedha kiholela huku akitambua ipo siku itafika atageukwa na wale watakaohitaji mfumo sahihi wa kuiongoza klabu ili yeye aingize faida na klabu pia ipate faida, mwisho wake i k a s h i n d i k a na akaamua k u j i o n d o a .
K u j i o n d o a kwa Manji n i l i t e g e m e a sasa wale w a l i o k u w a w a k i m p i n g a kwa nguvu zote na kumuona hafai basi wangeingia wao kwa kuwa wangekuwa wameshapata picha kuwa Manji anataka nini au alitaka kuifanyia nini Yanga.
Matokeo yake, Yanga imeendelea kuwa na hali ngumu, mara kadhaa wachezaji wameonyesha hilo kwa vitendo, lakini kukawa na siasa za hapa na pale kuonyesha kuwa kila kitu kiko sawa.
Yanga ni taasisi kubwa na katika dunia ya sasa unapoona klabu kama hiyo inakuwa na nafasi ya kufika mbali kutoka na maliasili watu iliyonayo, kisha wachezaji wakaendelea kulia njaa ni jambo baya kibiashara.
Najua kuna wapingaji wengi wa maendeleo kwa kuwa wanajua klabu kama Yanga au Simba inapoendelea kuwa na maisha ya kuungaunga ndiyo wao wanavyoendesha maisha yao, kwa mwendo ilionao ni kitu kibaya sana kwa Yanga kuendelea kulia njaa huku mtaji watu upo.