Zahera avunja na kuweka rekodi mpya Yanga

UKIWA ni msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amefanikiwa kuvunja rekodi ya kocha wa zamani wa timu hiyo, George Lwandamina kutokana na kushinda mfululizo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

Zahera, raia wa DR Congo, amevunja rekodi ya misimu miwili, kufuatia Yanga kushindwa kupata matokeo ya ushindi kwenye uwanja huo.

 

Ikumbukwe Yanga walishapoteza mechi tatu dhidi ya Mbao katika misimu miwili tofauti ndani ya uwanja huo. Mara ya kwanza walipoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA kwa kipigo cha bao 1-0 na mechi ya mwisho katika msimu wa 2016-17 kwa kipigo tena cha bao 1-0, kabla ya kupotea msimu uliopita kwa mabao 2-0.

 

Yanga ilipoteza mechi hizo ikiwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm kabla ya kuachana naye na kumchukua Mzambia, George Lwandamina lakini naye hakuweza kuifunga timu hiyo.

 

Lakini Zahera alianza kwa kuvunja rekodi ya Mbao kufuatia ushindi wa bao 1-0 kabla ya juzi Jumamosi kuweka rekodi mpya kwenye uwanja huo kutokana na kushinda mechi mbili za ligi mfululizo kwenye uwanja huo.

 

Ibrahim Mussa, dar es salaam

Toa comment