The House of Favourite Newspapers

Zahera: Molinga Asipofunga Mabao 20, Nikatwe Mkono

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo ametamba kwamba akatwe mkono mwishoni mwa msimu ikitokea straika wake, David Molinga asipofunga mabao 20 kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Zahera ameweka wazi kwamba anaamini straika wake huyo atafunga mabao mengi kwenye mechi za ligi kutokana na kufahamu kiwango chake ambapo alipokuwa DR Congo alifunga mabao mengi kuzidi straika wake aliyeondoka, Heritier Makambo.

 

Kocha huyo ameliambia Championi Ijumaa, kuwa Molinga atafanya makubwa na kufunga idadi kubwa ya mabao ambapo yeye anamuwekea kufunga mabao 20 kwani uwezo wake ni mkubwa zaidi kuliko Makambo ambaye ametua Horoya AC ya Guinea.

“Wakati Makambo ambaye wengi wanamsifia walipocheza na Molinga kule Congo alipitwa kimabao.
Makambo yeye alifunga mabao saba wakati Molinga alifunga mabao 15, sasa hapo utapima nani ni zaidi ya mwenzake. “Tena alifunga huko Congo kwenye timu kama TP Mazembe, AS Vita, DC Motema Pembe na nyinginezo. Ninasema kama Molinga asipofunga bao 15 au 20 kwenye ligi basi nikatwe mkono,” alisema Zahera.

 

KUTUPIA KIPENSI KAMA KAWAIDA Wakati akipigwa faini kutokana na mavazi yake ya ‘kipensi’ kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, Zahera ametamba kwamba kwenye mechi yao ya kesho Jumamosi ya Ligi ya Mabingwa
Afrika atatimba na kipensi chake kutokana na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kutompangia avae kitu gani.

 

Kocha huyo Mkongomani ameweka wazi kwamba kwenye mechi yao hiyo ya kesho dhidi ya Zesco United ya Zambia atatinga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar akiwa na kipensi chake ambacho amekuwa akivaa mara kwa mara.

 

“Kuhusu kuvaa kile kipensi nitaendelea kukivaa kwenye mechi yetu hiyo na Zesco kwa sababu huku sipangiwi nguo ambayo ninatakiwa kuivaa kwenye mechi.

 

“Nitakuja na mavazi hayo kwenye mechi hii ila ninataka watu watambue kwamba haya mavazi ambayo ninavaa ni ya gharama kubwa sana tofauti na vile watu wanavyochukulia. “Lakini juu ya hilo la mashabiki nao kuvaa ‘vipensi’ kwenye mechi hiyo kama wao wameamua kuvaa basi wavae, kila mmoja anaweza kuvaa atakacho,” alisema Zahera

Comments are closed.