The House of Favourite Newspapers

ZAMANI ‘HIT-SONG’, MSANII MKUBWA, SIKU HIZI KIKI KUBWA,‘HIT SONG’

Afande sele

ZAMA zinabadilika kwa kasi sana utadhani zinakimbizwa na mwanariadha mwenye heshima Bongo, Alphonce Simbu na walioushuhudia Muziki wa Bongo Fleva toka unaanza, kuna baadhi ya mambo ambayo wanayaona kwa sasa kwenye gemu wakawa wanacheka na kutikisa kichwa kwa maana ya kusikitika.

Wanasikitika kwa sababu mambo yamebadilika kabisa. Si kama zamani kwenye ‘era’ ya 2000, kipindi ambacho muziki wa Bongo Fleva ulikuwa na msisimko wa ajabu, ushindani mkubwa kuanzia kwa wanamuziki kazi zao, mpaka waandaaji wa kazi zenyewe.

Wakati huo ili mwanamuziki uwe mkubwa ulikuwa unapimwa una kazi gani kubwa! Ilikuwa raha sana kwa sababu mwanamuziki alikuwa anaweza kuibuka leo lakini kutokana na ukubwa wa kazi yake akawa staa, tofauti na siku hizi ili uwe staa kwa kiasi kikubwa unatakiwa kutengeneza kwanza kiki na ukubwa wa kiki yako ndiyo itatafsiri ukubwa wa wimbo wako na ustaa wako!

Hii hapa mifano michache ya wasanii wa zamani ambao ukubwa wa kazi zao uliwapa ustaa na nitakupa mifano ya siku hizi ya wasanii ambao ustaa wao umetokana na kiki zao!

DUDU BAYA VS SUGU

Wakati mwanamuziki Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya’ anaingia kwenye gemu Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alikuwepo kwenye gemu muda tu na alikuwa amekwisha tengeneza ‘hit song’ kadhaa na alikuwa na mashabiki wengi. Dudu Baya aliingia kama kimbunga. ‘Ile vuup’ na kuachia wimbo uitwao Mwanangu Huna Nidhamu. Wimbo huu ni miongoni mwa kazi bora kwenye ‘career’ yake kwani ulipokelewa vizuri sana.

Wimbo huu ndiyo ulimfanya kujulikana zaidi hasa aliposhindanishwa na Sugu kwenye kipindi cha Redio One cha Nani Zaidi na kupigiwa kura nyingi zaidi, hiyo ndiyo safari ya usataa wake ilipoanzia na baadaye akashika kabisa na nyimbo nyingi ikiwemo Nakupenda Tu!

AFANDE SELE VS SOLO THANG, PROFE-SSOR JAY

Wanamuziki hawa wote walikuwa ni wakali. Si Seleman Msindi ‘Afande Sele’, Msafiri Kondo ‘Solo Thang’ wala Joseph Haule ‘Professor Jay’. Kwa wanaokumbuka hata mashindano ya kumtafuta Mkali wa Rhymes ilikuwa ni kivumbi.

Wengi walimpa nafasi Professor Jay na nyimbo kali ikiwemo Msinitenge na wengine Solo Thang na ngoma kali kama Mpenzi na Nakuwaza lakini ‘hit song’ ambayo Afande alikuwa ameitoa ya Darubini Kali inatajwa kwa kiasi kikubwa kumpa taji hilo.

Baada ya Afande kushinda unaambiwa soko la albamu kwa wanamuziki wengi lilikufa kwa muda. Kila mtu sokoni alihitaji kupata albamu ya mfalme, na hiyo ni moja ya sababu ya wanamuziki wengine kugomea mashindano hayo baadaye.

DUDU BAYA VS MR. NICE

Baada ya kulishika gemu Dudu Baya aliendelea kuwa tishio kwa wanamuziki wengi. Kwa wanaokumbuka wakati Dudu alipokimbilia Kenya mwanzoni mwa miaka ya 2000 kwa ajili ya kusoma, aliporejea Mr. Nice ndiyo alikuwa mwenye gemu lake.

Ngoma za Kikulacho na Fagilia zilikuwa ‘hit song’ na zilikuwa zinasumbua kwenye chati mbalimbali ikiwemo chati ya 10 ya Ukumbi wa Billcanas ambayo ilikuwa ni moja ya chati ya muziki iliyoheshimika wakati huo na mwanamuziki wimbo wako ukiwa kwenye chati hiyo basi ni ‘hit song’.

Dudu Baya alipotoa Wimbo wa Mpenzi ukaenda na kumuangusha Mr. Nice kwenye chati hiyo, mfalme akawa amefuta vumbi kiti chake na kurudi kuwa juu tena, inaelezwa kwamba kutokana na Dudu kumuangusha Nice kwenye chati hiyo ndiyo ilikuwa chanzo cha bifu lao!

DAZ NUNDAZ VS EAST COAST, SOLID GRO-UND FA-MILY

Unalik-umbuka Kundi la Solid Ground Family? Big Black, Hama Guy na Master V! Lilikuwa ni kundi bora ambalo lilikuwa linachuana na makundi makubwa Bongo likiwemo Kundi la East Coast na mengine mengi.

Lakini kuibuka kwa Kundi la Daz Nundaz na kufanya vizuri kwa wana-muziki wengi wa kundi hili ni kama liliua makundi haya mengine. Daz Nundaz ikawa Daz Nundaz, homa ya jiji na kila mmoja alitamani kusikia kila ujio wao mpya unakuwaje.

SIKU HIZI SASA!

Kwa sasa mpaka Harmorapa ni staa. Nimem-shuhudia wikiendi hii akipiga shoo kwenye Ukumbi wa The Life, mpaka nikacheka. Mashabiki hawapigi shangwe kutokana na nyimbo zake kali ili wanapiga shangwe kumuona tu na kusikia maneno yake ambayo ameyazungumza mara kwa mara kwenye kiki zake.

Ndiyo maana tunasema mambo yanabadilika. Kiki zimetawala kwenye gemu, ndoa za ‘uongo na kweli’ zinafungwa kila mara na kuwahamasisha mashabiki kwamba baadhi ya wanamuziki wamefunga ndoa lakini unakuta hakuna lolote.

Watu wanaonyesha nyumba kali wakati mwingine ambazo siyo zao, mahusiano yanatengenezwa ili kubusti kazi na timu zinatengenezwa ili kuhakikisha mwanamuziki fulani tu anakuwa staa hata kama kazi yake si bora. Hizi ndizo zama za ‘digital’!

BONIPHACE NGUMIJE

 

Comments are closed.