The House of Favourite Newspapers

Zanzibar Yatwaa Tuzo Bab’Kubwa Tamasha la Filamu la Golden Globes 2019

 

FILAMU ya Bohemian Rhapsody inayohusu maisha ya muimbaji kinara wa bendi ya Queen ya Uingereza, Freddie Mercury,  ambaye ni mzaliwa wa visiwani Zanzibar imenyakua tuzo mbili kubwa za tamasha la filamu la Golden Globes.

 

Freddie Mercury ambaye ni mzaliwa wa Zanzibar.

 

Tuzo hizo zilitolewa usiku wa Jumapili, Desemba 6, kuamkia Jumatatu Beverley Hills, California,  nchini Marekani  ambapo filamu hiyo ilinyakua tuzo katika kipengele cha Filamu Bora ya Mwaka 2018 na Rami Malek ambaye ndiye alikuwa mhusika mkuu akiigiza kama Mercury amenyakua tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kiume.

 

Kava la Filamu ya Bohemian Rhapsody.

 

Filamu hiyo imejibebea umaarufu kwenye tamasha hilo kwani ilikuwa si matarajio ya wengi kutokana na kuipiga chini filamu ya Black Panther ambayo ilipata sapoti kubwa kabla na baada ya kuingia sokoni na mauzo yake kutingisha soko la filamu.

 

Rami Malek (aliye kifua wazi) akimwigiza Freddie Mercury katika filamu ya Bohemian Rhapsody.

 

Filamu nyengine zilizoshinda tunzo ni A Star Is Born ambayo ilipendekezwa sana lakini iliambulia tunzo moja tu. Huku filamu ya Green Book ilikua ni moja kati ya filamu kubwa zilizong’aa baada ya kung’oa tunzo tatu za filamu bora ya kuchekesha, mwigizaji bora msaidizi iliyoenda kwa mwigizaji Mahershala Ali na filamu iliyoandikwa vizuri zaidi.

 

Ushindi wa Bohemian Rhapsody unakuja kwa kishindo japokuwa kulikuwa na vikwazo vingi wakati wa utayarishaji wake.

 

Muongozaji mkuu wa awali wa filamu hiyo, Bryan Singer, alifukuzwa kazi kutokana na kile kilichotajwa kuwa “tabia zisizovumilika” na kuibua taarifa kuwa alikuwa na mifarakano na Malek wakati wakiandaa filamu. Dexter Fletcher aliletwa baadaye ili kumaliza utayarishaji wa filamu hiyo.

 

Bryan Singer.

 

Filamu hiyo imevuma sana na kufanya vizuri katika mauzo sokoni na sasa jina la Malek litaingia katika majina yaliyopendekezwa kwa  tuzo maarufu zaidi za Oscar baadaye mwezi huu.

 

Katika hotuba yake wakati akipokea tuzo hiyo Jumapili usiku, Malek hakumshukuru Singer, lakini badala yake alitoa heshima kwa bendi ya Queen na kusema kuwa amejawa furaha sana kwa ushindi huo.

 

“Kwako, Brian May, kwako, Roger Taylor, kwa kuhakikisha kwamba uhalali na uhalisia unabaki duniani,” alisema. Wote May na Taylor ambao ni waasisi wa bendi hiyo walihudhuria sherehe hizo.

 

Alielekeza tuzo hiyo kwa Mercury, ambaye alifariki mwaka 1991, na kuongeza: “Hii na kwa ajili yako na kwa sababu yako!”

 

Mercury ndiye alikuwa kiongozi wa bendi hiyo ya Queen, ambapo filamu hiyo iliakisi zaidi maisha yake.

 

Kile ambacho wengi hawakifahamu na hakizungumziwi sana katika filamu hiyo ni kuwa alizaliwa katika visiwa vya karafuu vya Zanzibar kwenye familia ambayo asili yake ni India na Uajemi. Jina lake alilopewa na wazazi ni Farrokh Bulsara, na baadaye akabadili kuwa Freddie Mercury.

 

Nyumba ya familia ya Freddie Mercury walikuwa wanaishi Zanzibar.

 

Mercury alizaliwa katika hospitali ya serikali huko Zanzibar tarehe 5 Septemba mwaka 1946. Wazazi wake Bomi na Jer Bulasara wana mizizi yao huko Uajemi lakini walikuwa pia wameishi nchini India.

 

Bomi Bulsara alitokea huko Bulsar Gujarat (ndiyo maana familia ina jina hilo) na kuhamia Zanzibar alikofanya kazi kwenye mahakama kuu kama karani wa serikali ya Uingerezea.

 

Alimuoa Jer huko India na kumleta Zanzibar. Farrokh, mtoto wao kifungua mimba, alifuatwa miaka sita baadaye na binti yao, Karishma.

 

Mercury mara nyingi hakuongea hadharani kuhusu malezi yake huko Zanzibar ambako waliishi kwenye nyumba nzuri iliyokuwa ikiangalia baharini kwenye mji wa Stone Town ambayo ni sehemu ya kihistoria ya mji wa Zanzibar.

 

Mtaa wa Stone town ambao mwimbaji huyo maarufu alikulia.

Leo hii mashabiki wake wanaweza kutembelea sehemu alizokulia ikiwemo nyumbani kwake na mahakama ambapo baba yake alifanya kazi. Pia kuna mgahawa uitwao Mercury’s.

 

Miaka ya kwanza ya masomo ya Mercury ilikuwa  katika shule ya Wamishenari huko Zanzibar ambapo alifundishwa na watawa wa Kianglikana. Lakini akiwa na umri wa miaka minane wazazi wake waliamua kumpeleka shuleni huko India.

 

Alisomea shule ya St Peter’s Church of England huko Panchgani kusini-mashariki mwa mji wa Bombay (sasa Mumbai).

 

Wakati akiishi na shangazi na mababu zake huko Bombay ndipo akagundua kuwa aliupenda muziki abako aliunda bendi yake ya kwanza ya Hectics.F

 

Freddie alirejea Zanzibar 1963, mwaka ambao visiwa hivyo vilipata uhuru kutoka Uingereza na kumalizia masomo katika shule ya Kikatoliki ya St Joseph’s Convent School.

 

Rafiki yake mmoja kutoka nyakati hizo anakumbuka jinsi walikuwa wakiogelea baharini baada ya kutoka shuleni na pia walivyokuwa wakiendesha baiskeli ufukweni sehemu za kusini.

 

Lakini nyakati nzuri zilikuwa fupi. Mwaka 1964 Mapinduzi yaliwatimua Waarabu waliokuwa wanatawala ambapo yakisiwa watu 17,000 waliuawa. Jamhuri ikaundwa na marais wa Zanzibar na Tanganyika, ambapo kwa kusaini mkataba wa umoja wakaunda Jamhuri ya Muungano Tanzania.   Familiia ya Bulsara na wengine wengi wakakimbia visiwa hivyo.

Freddie Mercury (wa pili kushoto) akiwa na wanamuziki wa bendi ya Queen mwanzoni mwa miaka ya 1970.

 

Baadhi ya washindi wa tuzo za Golden Globes 2018

  • Filamu bora – Bohemian Rhapsody

 

  • Filamu bora vichekesho au muziki – Green Book

 

  • Mwigizaji bora wa kiume – Rami Malek (Bohemian Rhapsody)

 

  • Mwigizaji bora wa kike – Glenn Close(The Wife)

 

  • Mwigizaji bora wa filamu/muziki – Christian Bale(Vice)

 

  • Mwigizaji bora wa kike filamu/muziki – Olivia Colman(The Favourite)

 

  • Tamthilia bora – The Americans

 

 

 

Comments are closed.