visa

Zari Atinga Uganda Kumtambulisha King Bae

KWA mara nyingine, mwanamama mjasiriamali Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, ameibua gumzo baada ya kutinga nchini kwao, Uganda kwa ajili ya kumtambulisha anayedai ni mumewe almaarufu kwa jina la King Bae. 

 

Vyombo vya habari nchini humo, juzi viliripoti kuwa Queen Bae wakimaanisha Zari na King Bae walikuwa jijini Kampala, Uganda wakitokea maskani kwao nchini Afrika Kusini ‘Sauz’.

 

Zari alionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe jijini Kampala ambapo alipokelewa na gari alilokuwa akilitumia aliyekuwa mumewe, marehemu Ivan Ssemwanga lenye pleti namba ya jina la IVAN9.

 

Awali haikufahamika vyema kama Zari na King Bae walitua na ndege moja, lakini uchunguzi ulibaini kwamba, wawili hao walifika na ndege tofauti.

 

Baada ya wawili hao kupokelewa kwa wakati tofauti kisha wakaungana pamoja, jambo zuri ambalo lilimfurahisha Zari ni namna ambavyo kuna mtu alikuwa akimfundisha King Bae lugha mbalimbali kama Luganda, Lusoga na Kiswahili.

Zari ambaye ni mama wa watoto watano wakiwemo wawili aliozaa na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ alionekana kuwa na furaha muda wote huku akitupia mtandaoni video iliyomziba King Bae asionekane laivu. “Haloo Uganda! Queen Bae (Zari) yupo hapa,” aliandika Zari kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

 

Zari yupo kwenye ziara hiyo ya Uganda inayotajwa lengo lake ni kumtambulisha King Bae ukweni na baada ya hapo anaelekea nchini Kenya kuungana na rafiki yake, Akothee kwa ajili ya mkutano wao wa kuwezesha wanawake nchini humo.

 

Ni takriban mwezi mmoja tangu Zari alipodai kufunga ndoa ya siri na King Bae huko nchini Afrika Kusini. Zari na King Bae au Mr M wamekuwa kwenye mapenzi Februari 14, mwaka huu alipomtambulisha rasmi jamaa huyo ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipoachana na Diamond au Mondi.

 

Wakiwa Uganda, King Bae alitarajiwa kukutana na baba wa Zari, Hassan Tiale ambaye tayari alikuwa jijini Kampala baada ya kupewa taarifa kuwa jamaa huyo atafika ukweni ambapo watasafiri hadi Jinja, sehemu Zari aliyozaliwa na kukulia.
Toa comment