The House of Favourite Newspapers

ZENGWE MAGARI YA MASTAA, LULU DIVA FUNIKA, WEMA AWEKA REKODI

DAR ES SALAAM: NI zengwe limeibuka! Magari ya kifahari wanayotumia mastaa yameibua zengwe la aina yake ikidaiwa kuwa wengi wao, hawana uwezo wa kuyanunua kutokana na kuwa na vipato vya kawaida.

 

SIRI YAFICHULIWA

Mtu wa karibu na mastaa hususan wa kike, ameeleza kuwa, mastaa wengi mjini wamekuwa na tabia ya kukodisha magari ingawa hujifanya ni ya kwao na wamekuwa na makubaliano maalum ya kuendesha wenyewe licha ya kwamba wanakodisha.

“Yaani wanakodisha tena wengi wao hujifanya ni yao kabisa na si rahisi sana mtu kugundua kwa sababu wanakaa nayo muda mrefu hivyo kwa mashabiki si rahisi kuwagundua,” alidai mtu huyo.

 

WENYEWE WANAJUANA

Hata hivyo, mtu huyo alilieleza Amani kuwa mastaa wengi wanajuana juu ya wale wanaomiliki magari kwa maana ya kuwa na kadi zenye majina yao lakini pia anayo listi ya mastaa wengi ambao magari yao ni ya kuazima. “Wapo kweli ambao wanazo kadi za magari yao lakini wapo wengi pia ambao kadi hazina majina yao, wanaazima na ndio maana baada ya muda fulani huwaoni nayo,” alisema.

 

Amani lilipojaribu kumdodosa mtu huyo, hakutaka kuwataja wale mastaa ambao kadi hazisomi majina yao kwa kile alichosema ni rahisi kumtambua kuwa yeye ndiye aliyevujisha habari lakini hata hivyo, alikuwa tayari kuwataja wale ambao magari yao wanayamiliki kwa kuwa kadi zenye majina yao.

 

“Mtu kama Aunt Ezekiel, Wema Sepetu, Shilole (Zuwena Mohammed), Kajala Masanja na Lulu Abbas ‘Lulu Diva’ hawa magari yao ukiyachunguza utakuta majina yao halisi yapo kwenye kadi lakini wengi wao ndio hivyo magumashi tupu,” kilidai chanzo hicho.

 

AMANI MZIGONI

Licha ya kutajiwa wasanii hao ambao magari yao yana kadi zinazosomeka majina yao, Amani liliingia mzigoni na kuyachimba magari yao ili kujiridhisha kama ni kweli wasanii hao wanayamiliki kwa majina katika kadi pamoja na wale ambao hazisomi majina yao.

MAGARI YENYEWE

Amani lilijiridhisha pasi na shaka kwamba, Aunt anamiliki magari mawili; Toyota Porte (sh. Mil. 10) na Toyota Alphard (sh. Mil. 20 ambayo yote yanasomeka majina yake.

WEMA

Kwa upande wake Wema, Amani lilijiridhisha anamiliki gari aina ya Toyota Crown Majesta ambalo lina thamani ya shilingi milioni 14 ambapo inasoma jina lake.

KAJALA

Kajala ilibainika kuwa anamiliki gari aina ya Toyota Harrier ambayo ina thamani ya shilingi milioni 30.

SHILOLE

Mrembo huyo ilibainika kuwa anamiliki kihalali gari aina ya Toyota Rush yenye thamani ya shilingi milioni 10.

LULU DIVA FUNIKA BOVU

Mrembo ambaye alionekana kuwafunika mastaa wengi Bongo kwa kuwa na mkoko wa maana ambao unasoma jina lake ni Lulu Diva ambao una thamani ya shilingi milioni 90. Licha ya kuwepo kwa fununu nyingi kuhusu nani aliyempa jeuri hiyo lakini mrembo huyo ameweka wazi kuwa muziki na biashara zake ndivyo vimemfanya aendeshe gari hilo la ndoto yake.

AMANI KUCHIMBA ZAIDI

Licha ya Amani kujiridhisha kwa mastaa hao, kutokana na mastaa wengi kudaiwa kutumia magari ambayo hayana majina yao, juhudi za gazeti hili hazikufanikiwa kuwanasa hivyo uchunguzi zaidi unaendelea.

WEMA AWEKA REKODI

Amani lilibaini katika warembo wote hao, mrembo ambaye ameweka rekodi ya aina yake katika kubadilisha magari ni Wema ambapo kabla ya kumiliki Crown ya sasa, amewahi kumiliki magari mengine sita ya gharama lakini aliyauza huku mengine ikidaiwa kuwa alikuwa akipewa na wapenzi wake kisha baadaye kupokonywa.

Aliwahi kumiliki Toyota Lexus (mil. 40), Toyota Mark X (mil.35), Audi Q7 (mil. 80), BMW 545i (mil. 45), Nissan Murano (mil.36) na Range Rover Evogue (mil.140). Aidha, Amani limebaini kuwa, wapo mastaa wengi wanaomiliki magari kihalali lakini asilimia kubwa magari hayo wameyapata kutokana na jeuri za wapenzi wao

Comments are closed.