The House of Favourite Newspapers

ZIC Yajipanga Kuadhimisha Miaka 53 Kwa Mafanikio Makubwa

0
Mkurugenzi wa Bima ya Kawaida wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Bw Jape Khamis (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mipango ya shirika hilo kuelekea maadhimisho ya miaka 53 tangu kuanzishwa kwake jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni pamoja na Ofisa Masoko na Mahusiano wa benki hiyo Bw Mohammed Shabani (Kulia) na Ofisa Mauzo wa Shirika hilo Bi Victoria Mwampogo

Kuelekea maadhimisho ya miaka 53 tangu kuanzishwa kwake, Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), limeandaa matukio kadhaa ikiwemo kutoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja iliyopo visiwani Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Bima ya Kawaida wa ZIC, Bw Jape Khamis alisema mbali na msaada huo shirika hilo pia limejipanga kutoa zawadi ndogo ndogo kwa wateja wake katika kipindi cha wiki moja kote nchini ambao watakata bima kupitia ofisi za kanda au kupitia kwa wakala wa shirika hilo .

”Zoezi hili la utoaji wa zawadi linaanza leo Juni 13 na litaendelea hadi Juni 20 mwaka huu. Zawadi zitakazotolewa ni zile za kustukizwa yaani ‘surprise gifts’ ’’ Alisema Bw Cheo

Akizungumzia tukio la utoaji wa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja iliyopo visiwani Zanzibar Bw Jape alisema tukio linalotarajiwa kufanyika Juni 18, ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wateja wa shirika hilo katika kuboresha sekta ya afya visiwani humo.

“Kupitia wananchi hawa, ndipo biashara yetu inapofanikiwa na hivyo tuna wajibu wa kuchangia maendeleo ya nchi hii kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya. Changamoto za sekta ya afya kwetu ni jambo la kipaumbele, kwa kuwa afya ndio msingi wa uchumi na uzalishaji mali na ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya wananchi” alisema.

Kuhusu tukio la tatu ambalo ni kilele cha maadhimisho ya miaka 53, Bw Jape alisema shirika hilo limeandaa hafla maalum likilenga kukutana na wateja wake katika hoteli ya Golden Tulip Airport Hotel iliyopo visiwani humo kwa ajili ya kujipongeza kwa pamoja, kupata mrejesho kutoka kwa wateja kuhusu huduma zake, kujadili fursa za biashara pamoja na kuzindua huduma mpya za bima zikiwemo huduma za Tour Operator Insurance, Travel Insurance pamoja na Program maalum ya mtandaoni kwa ajili ya huduma za shirika hilo yaani Online Application.

“Kupitia App hii ya ZIC wateja wetu wataweza kupata huduma zote za msingi tunazozitoa ikiwemo kukata bima pamoja na kujifunza mengi kuhusu huduma na shirika kwa ujumla kupitia simu zao za mkononi …haya ni mapinduzi makubwa ya kibiashara na kihuduma hivyo tunahitaji kujipongeza na wateja wetu huku pia tukitoa fursa ya wao kukutana na kubadilishana fursa mbalimbali baina yao yaani business networking jioni hiyo,’’ alisema.

Alitoa wito kwa wadau na wateja wa shirika hilo kote nchini kuwaonga mkono katika maadhimisho hayo kwa kuendelea kutumia huduma za shirika hilo ikiwemo Appilication ya ZIC ambayo inalenga kuwarahishia uapatikanaji wa huduma zake bila kutembelea ofisi za shirika hilo.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply