The House of Favourite Newspapers

Zitto Kabwe, Freeman Mbowe Wamvaa DPP Bungeni – Video

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), ameishutumu Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP), kwamba imekuwa na utaratibu wa kukubaliana na wahalifu na kuwatoza faini ili makosa yao yafutwe hata kama wana mashtaka mahakamani.

Kutokana na hali hiyo, ameitaka Serikali itoe ufafanuzi ni kwanini ofisi hiyo inakubaliana na wahalifu hao. Zitto ameyasema hayo bungeni leo Ijumaa Aprili 12, alipokuwa akichangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Tamisemi, Utawala Bora pamoja Utumishi wa Umma.

 

Akitoa mfano Zitto amesema kesi za watumishi wa Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, ambapo watumishi wake waliokuwa na kesi mahakamani kwa kosa la utakatishaji fedha waliachiwa baada ya mazungumzo kufanyika.

“Kumekuwa na utamaduni ofisi ya mwendesha mashtaka kukamata watu, hatujui kama wanabambikiwa kesi au la, lakini baadaye tunaona watu wale wanakubaliana na ofisi ya DPP na kulipa pesa na kesi hiyo inakwisha,” amesema Zitto.

“Ningependa nchi yetu ipate ufafanuzi huenda kuna uonevu mkubwa sana, kwamba watu wanabambikiwa kesi kwa utakatishaji fedha wanawekwa ndani ili wazungumze na DPP halafu waende mahakamani wakiri na kulipa faini kiwango ambacho wameshtakiwa nacho.”

“Nchi yetu haina sheria wala kanuni zinazowezesha pale ambapo mtu ametuhumiwa kujadiliana na mwendesha mashtaka ili ama kupunguza adhabu, kufuta adhabu au kulipa faini, haya makubaliano ya DPP na watuhumiwa yanaendeshwa kwa sheria ipi?”

 

Amesema mwaka jana DPP amekusanya zaidi ya Sh23bilioni kwa watu wanaokamatwa  na kumaliza kesi kati yao na DPP, “Tunaomba kufahamu kwa sheria ipi? Fedha zinakwenda wapi na nani anakagua hizo fedha. Hatuwezi kuendesha nchi namna hii naomba tupate maelezo.”

 

Wakati Zitto akisema hayo, Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema), amesema utaratibu huo wa Ofisi ya DPP kukubaliana na watuhumiwa unawatisha wawekezaji kwa kuwa haufuati utawala bora.

 

Katika maelezo yake, Mbowe alitolea mfano Mbia wa serikali katika mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam, Simon Kisena ambaye ana kesi mahakamani.

 

Kwa mujibu wa Mbowe serikali ingeweza kuzungumza na Kisena na kumaliza tofauti zilizopo kwa vile wana ubia katika mabasi hayo. Wakati huo huo, Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), aliitaka ofisi hiyo ya DPP iwe na utaratibu wa kuwaachia watuhumiwa wasiokuwa na makosa badala ya kuendelea kuwashikilia bila sababu.

Comments are closed.