The House of Favourite Newspapers

Maamuzi ya Mahakama Kuu Kesi ya Zitto na Wenzake Vs Mwanasheria Mkuu – Video

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (watatu kulia) Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Vincent Mashinji (wapili kushoto) wakitinga Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam leo Januari 4, 2019, imeahirisha kesi No. 31 ya mwaka 2018, ambayo imefunguliwa na Kiongozi wa ACT Wazalerndo, Zitto Kabwe na wenzake wawili dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiitaka mahakama kuzuia kusomwa bungeni mara ya pili kwa muswada wa sheria ya vyama vya siasa.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (watatu kulia) Katibu mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Vincent Mashinji (wapili kushoto) wakitinga Mahakama Kuu ya Tanzania.

Katika kesi hiyo ambayo vyama 10 vya upinzani vimeungana kufungua jalada hilo mahakamani hapo huku walalamikaji wakiwa ni Zitto, Joran Lwehabula Bashange na Salim Abdallah Rashid Bimani wote wa Chama cha Wananchi (CUF) imeahirishwa hadi saa 8 mchana leo ambapo Mahakama hiyo itatoa uamuzi.

Rungwe akisalimiana na viongozi wengine wa vyama vya upinzani katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akitoa maelezo mahakamani hapo, wakili wa Serikali ameiomba Mahakama kuongezewa muda wa siku 21 ili kuwasilisha utetezi wao lakini mawakili wa upande wa utetezi wameomba wapewe siku chache zaidi sababu muswada utawasilishwa bungeni Januari 15, mwaka huu.

Rungwe (wapili kulia) akiwa kwenye chumba cha Mahakama Kuu kabla ya kesi kuanza

Mawakili hao wamesema ili kuzuia muswada kupelekwa bungeni mahakama itoe muda mchache zaidi, na endapo siku 14 zitatolewa basi mahakama imeombwa kutoa zuio kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupeleka muswada huo bungeni sababu serikali ndiyo inayomiliki muswada. 

Taswira ilivyoonekana mahakamani hapo.

 

Kutokana na hoja hizo na nyingine zilizotolewa mahakamani hapo, Mahakama imesema ikapanga kutoa maamuzi saa 8 mchana wa leo.

 

Akizungumza jana, Zitto alisema wamefungua kesi hiyo wakiiomba mahakama kuzuia Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kwa madai kuwa unakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake na kwamba muswada huo unafanya shughuli za kisiasa kuwa suala la jinai.

Ndani ya chumba cha Mahakama Kuu.

Aidha, Zitto alisema Muswada huo unalenga kumfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na Mamlaka ya Usimamizi (Regulatory Authority), kuwa na mamlaka ya kuingilia shughuli za kiutawala na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo kusimamisha/ kumfukuza mtu uanachama.

 

UPDATES:

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya DSM katika Kesi Na. 31 ya 2018 – Zitto Kabwe, Salim Bimani & Joran Bashange v/s Mwanasheria Mkuu wa Serikali – imetoa ruling kwamba Mawakili upande wa Serikali wanapaswa kuwasilisha utetezi wao wa maandishi ndani ya siku 7 kuanzia leo.

 

Kwa ruling hiyo, Mahkama imekataa ombi la Mawakili wa Serikali waliotaka wapewe siku 21 kuwasilisha utetezi wao wa maandishi. Kwa siku 7 walizopewa wametakiwa wawe wamewasilisha utetezi wao ifikapo tarehe 9 Januari ili Mahkama isikilize kesi tarehe 11 Januari, 2019.

 

Mahkama imesema maombi ya kumzuia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuuwasilisha mswada Bungeni kwa sasa hayahitajiki, kwa sababu kesi itasikilizwa tena tarehe 11 Januari, 2019 kabla ya Mswada kuwasilishwa kwa kusomwa kwa mara ya pili tarehe 15 Januari, 2019.

 

NA DENIS MTIMA | GPL

Comments are closed.