The House of Favourite Newspapers

Uvuvi Haramu… Bwawa la Nyumba ya Mungu Lafungwa

1

915516541

Wavuvi katika Bwawa la Numba ya Mungu.

Mwanga: Serikali imesitisha kwa mwaka mmoja shughuli za uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu linalotegemewa na wavuvi wa mikoa miwili ya Kilimanjaro na Manyara kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu.

Kufungwa kwa bwawa hilo ambalo sasa samaki wanaovuliwa ni wadogo, kutakuwa na athari za kiuchumi si kwa wavuvi tu, bali pia wafanyabiashara na walaji.

Uamuzi wa kufungwa kwa bwawa hilo linalotegemewa na wananchi wa vijiji vya Wilaya za Mwanga na Moshi mkoani Kilimanjaro na Simanjiro mkoani Manyara ulitangazwa na Serikali juzi.

Akitangaza maazimio 14 ya wadau wa bwawa hilo waliokutana Mwanga, Katibu Tawala (Ras) wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi alisema bwana hilo litafungwa kuanzia Julai Mosi hadi Juni 2017.

BWAWABwawa la Nyumba ya Mungu.

]Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki na wa Manyara, Joel Bendera, wadau walikiri hali ni mbaya katika bwawa hilo kutokana na uvuvi haramu.

Uvuvi huo haramu umesababisha samaki wanaovuliwa kushuka kutoka tani 25,000 mwaka 1970 hadi tani 11 mwaka 2016. Taarifa zinasema kiwango kimekuwa kikishuka taratibu kuanzia mwaka 1973.

Maswi alisema katika maazimio hayo, viongozi wa vijiji na kata wakishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, wametakiwa kuwabaini wanaomiliki nyavu aina ya makokoro ifikapo Juni 30 mwaka huu.

Kadhalika, Serikali imetoa muda wa mwezi mmoja hadi kufikia Juni 30 wamiliki wote wa makokoro kuyasalimisha kwa hiyari kwa vyombo vya dola na kwamba wasiofanya hivyo watakamatwa.

Chini ya maazimio hayo, wavuvi wote watakaosalimisha makokoro hayo kwa hiyari, watasainishwa mkataba wa kutorudia tena kuvua kwa kutumia nyavu hizo na wakirudia watafikishwa kortini.

Akizungumza katika mkutano huo, Bendera alisema katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, Serikali haitaruhusu aina yoyote ya uvuvi na mvuvi atakayeonekana ndani ya bwawa hilo atakamatwa.

“Mvuvi yeyote atakayeonekana ndani ya Bwawa la Nyumba ya Mungu atakamatwa. Ni lazima tukubali kunywa dawa chungu ya mwaka mmoja lakini tupate samaki wakubwa baadaye,” alisema Bendera.

Akisisitiza, Sadiki alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinasajili mitumbwi yote itakayoruhusiwa kuingia ndani ya bwawa baada ya kufunguliwa Julai 2017.

Baadhi ya wananchi wanaotegemea uvuvi kujikimu kimaisha, walisema hatua hiyo itawaathiri kimaisha kwa kuwa bwawa hilo ndilo shamba lao lakini wanaafiki uamuzi wa Serikali.

1 Comment
  1. […] ya Uvuvi wa Bahari Kuu na wadau kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Bara) […]

Leave A Reply