The House of Favourite Newspapers

Big; Baharia Aliyepotezwa na Dili za Magari

0

NAAM mpendwa msomaji wa kolamu hii ya Yupo Wapi, leo nimekuletea mkali wa Bongo Muvi, Lumole Matovolwa maarufu kama Big.

Big ametamba na filamu mbalimbali kama Sabrina, Girl Friend, Saa 24, Baamedi, Mdundiko na nyinginezo.

 

Mwanahabari wetu alipobambana na Big baada tu ya salamu, maswali ya fastafasta yalianza.

Risasi: Big kwanza mashabiki wako wangefurahi kujua umezaliwa lini na wapi?

Big: Nimezaliwa Hospitali ya Ocean Road hapa Dar, tarehe 29 Oktoba 1976.

 

Risasi: Dah! Kumbe wewe ni mtoto wa mjini, vipi kiasili ni mtu wa wapi?

Big: Kiasili mimi ni Mnyamwezi wa Sikonge mkoani Tabora, ndipo walipotoka wazazi wangu kabla ya kuja Dar, kuanza maisha.

Risasi: Kipaji chako cha uigizaji kiliibukia wapi?

 

Big: Kipaji changu cha uigizaji kilianza kuibuka katika kundi la Mwana Arts lililokuwa pale Mwananyamala mwaka 2001 na baadaye mwaka 2002 nilipojiunga na Kundi la Nyota Academy ndipo nikaanza kuwa staa.

 

Risasi: Miaka hiyo ulikuwa na kina nani ambao nao walikuwa wakiusaka ustaa na wakaupata?

Big: Duuh! Pale tulikuwa mimi, George Tyson, Monalisa, Natasha, Benny Kinyaiya, JB na Ray kabla hajaenda Kaole na wengine wengi tu ambao tuliopatia ustaa pale.

Risasi: Sasa mashabiki zako wanasema umepotea sana kwenye gemu la filamu kwa hivi karibuni, hilo likoje?

 

Big: Hilo ni kweli, kilichonipoteza kwenye filamu ni kazi hiyo kutolipa, hivyo nimeamua kuanzisha biashara ya kukodisha magari na hiyo ndiyo kazi inayoniweka mjini kwa sasa. Wasanii wengi wa filamu sasa hivi wamekuwa wakitegemea zaidi kuitwa kwenye hizi tamthiliya ndiyo kidogo zinawalipa vizuri lakini siyo utegemee kuchezeshwa filamu, utakufa njaa.

 

Risasi: Magari ya aina gani unayokodisha?

Big: Nina gari za aina mbalimbali, hizi ndogo kama vile Noah, Toyota Colora Ti na nyinginezo ambapo nazikodisha kwa wenye masherehe na watu wenye mahitaji mbalimbali.

Risasi: Vipi kuhusu familia umeoa?

 

Big: Nimeona na nina watoto wawili Talhiya (10) na Rawhiya (5).

Risasi: Ukiachana na uigizaji, una taaluma gani nyingine.

Big: Mimi ni baharia, nilisomea pale, Dar es Salaam Marine Institute (DMI) na nimefanya kazi ya ubaharia kwa muda mrefu. Meli yangu ya mwisho kufanya nayo kazi ni Linea Messina iliyokuwa ikipiga safari za Dar, Mtwara, Mombasa na sehemu nyingine.

 

Risasi: Unalizungumziaje jina la ubaharia linavyotafsiriwa mitaani kwa sasa?

Big: Wanalipotosha sana kwa kulipa sifa zingine ambazo ni tofauti kabisa na matendo ya kibaharia.

Risasi: Ok, Sawa Big piga kazi, natumaini mashabiki zako watajua mengi dhidi yako kutokana na mazungumzo yetu haya.

Makala: Richard Bukos

Leave A Reply