The House of Favourite Newspapers

Maajabu Kabila Linalokula Nyama za Watu! – 5

0

BAADA ya kuona makabila ya Kuru na Wakorowai yanayopatikana kwenye Visiwa vya Papua New Guinea namna yanavyokula nyama ya binadamu wenzao, wiki hii tunamalizia simulizi hii kwa kulitazama kabila lingine linalopatikana kwenye visiwa hivyo.

Kabila lingine maarufu linalokula nyama za binadamu visiwani humo ni Wafore.

Kabila hili lilikuwa halijulikani hadi miaka ya 1950 baada ya watafiti kuwafanyia utafiti huku watafiti hao wakiwa kwenye hatari ya kuuawa na kuliwa miili yao.

Wakati wa utafiti huo, waligundua kuwa watu hao walikuwa wakila wenzao waliokuwa wakifariki dunia, hivyo kujikuta wakikumbwa na maradhi yaliyoitwa ugonjwa wa kifo cha kucheka; yaani laughing death.

Ugonjwa huu uliua wanawake na watoto wengi sana kutokana na kula nyama za watu.

Walikuwa wanakula miili ya wenzao waliokufa, badala ya kuwazika, wakawafanya kitoweo kwa madai ya kwamba walikuwa wakiwaokoa wapendwa wao hao ili wasiliwe na funza pindi watakapooza.

Nyama ya miili ya watu walikuwa wakiita ‘nyama ya nguruwe mrefu’ yaani long pig.

Wafore walisema ni bora miili hiyo ikaliwa na wao na ikae kwenye matumbo yao badala ya kuliwa na funza kwa madai kwamba roho zao zitazidi kuishi kwenye matumbo yao hasa ya wanawake.

Kwa imani hiyo, wanawake walikuwa wakipewa ubongo waupike na kuula kisha nyama kutengenezwa ‘rosti’, hivyo kula na watoto wao.

Hata hivyo, ulaji huo wa miili ya wenzao pamoja na ubongo ulifanya wapate maradhi ambayo yaliua watu wengi wa jamii hiyo. Mtu aliyekuwa akipata ugonjwa huo alikuwa anapoteza nguvu na kushindwa kutembea kisha mwili kukonda.

Mtafiti aliyeitwa Dk Jekly alisema kilichokuwa kikisababisha maradhi hayo siyo bakteria au virusi isipokuwa protini iliyokuwa kwenye ubongo wa maiti ambayo ikiliwa ilikuwa inaharibu ubongo kwani ilikuwa inasababisha kucheza au kutikisika na kuharibika, jambo ambalo kitaalam huitwa brain’s cerebellium.

Ugonjwa huo uliwaandama sana watu hao wala miili ya watu hadi mwaka 2009 ambapo mtu mmoja aliripotiwa kufariki dunia kwa maradhi hayo.

Lakini tukio baya lilitokea Julai, 2012 ambapo watu 29 wa makabila hayo waliwala watalii kwa kupika miili yao huku wanaume wakitengeneza supu ya sehemu nyeti na ubongo.

Kitendo hicho kilisababisha Serikali kuingilia kati na kwa mujibu wa Gazeti la The National Newspaper la huko, Kamanda wa Polisi Madang, Anthony Wagambie alithibitisha kutokea kwa matukio hayo.

“Huwa hawafikirii kwamba wanafanya kitu kibaya, wanakiri hayo waliyoyafanya waziwazi,” alisema kamanda huyo.

Alisema wauaji wanaamini kuwa waliowaua walikuwa wachawi ambao kwa kabila lao huitwa Sanguma na kwamba walikuwa wakiwapa kilevi wenyeji huku wakifanya mapenzi na wanavijiji maskini kwa njia ya kishirikina.

Kwa kula viungo vya binadamu, waganga wao walikuwa wanawaambia kuwa watapata nguvu ya ajabu na kwamba hata wakipigwa risasi, hazitaingia kwenye miili yao.

Kamanda Wagambie alisema waligundua kulikuwa na kundi la watu kati ya 700 na 1,000 wa vijijini Kaskazini Mashariki ambao walikuwa wana imani hiyo.

Alisema walikamata watu 28, wake kwa waume na waliwapandisha mahakamani kujibu tuhuma za mauaji ya binadamu wenzao. Waliopatikana na hatia, walihukumiwa adhabu ya kifo.

Akasema watuhumiwa wote waliwaweka rumande na kuendelea kuwatafuta wengine waliokula nyama za watu.

Alisema watu hao walifanya ukatili mkubwa kwa kuwaua watalii saba na anaamini kwamba walikula miili yao.

-MWISHO-

 

 MTEMBEZI…

Msimuliaji: Sifael Paul

0713 750 910

Leave A Reply