The House of Favourite Newspapers

Cannavaro aanza kuogopa Yanga SC

0

CANA
Omary Mdose,
NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ameogopa na kusema msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaweza kuwa mgumu kwao hata kutetea ubingwa kwani wana uchovu wa kucheza mechi nyingi mfululizo.
Cannavaro amesema hayo wakati Yanga ikiwa bado kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Tofauti na timu nyingine za ligi kuu ambazo zilipumzika baada ya ligi hiyo kumalizika Mei, mwaka huu, Yanga yenyewe iliendelea na mechi za Kombe la Shirikisho na itacheza hadi Agosti 24, mwaka huu.
Yanga inatarajiwa kumaliza mechi zake za Kundi A za Kombe la Shirikisho kati ya Agosti 23 na 24, mwaka huu wakati msimu ujao wa ligi kuu ukianza Agosti 20, yaani siku tatu au nne nyuma yake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Cannavaro alisema msimu uliopita walipata muda wa kupumzika na wakatetea vizuri ubingwa wa ligi kuu, lakini safari hii hawajapumzika na mambo yanaweza kuwa magumu.
“Tangu ligi imalizike hatujapumzika, halafu ukiangalia msimu mpya unatarajia kuanza, hii itatufanya tuwe na wakati mgumu wa kutetea ubingwa wetu kwani tutakuwa tumechoka,” alisema Cannavaro.
Kuhusu Yanga kutofanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho, Cannavaro alisema: “Kinachotuangusha ni kushindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani, wenzetu wakicheza kwao wanapata matokeo mazuri lakini kwetu inakuwa tofauti.
“Hili ni somo kwetu na kwa kuwa msimu ujao tutashiriki tena, basi tutafuta makosa yetu, benchi la ufundi nadhani limeona linatakiwa kusajili wachezaji wa aina gani hasa katika michuano hii ya kimataifa.”
Yanga inashika mkia katika kundi lake ikiwa na pointi moja tu huku TP Mazembe ikiwa kinara na pointi 10 ikifuatiwa na Medeama na MO Bejaia ambazo kila moja ina pointi tano.

Leave A Reply