The House of Favourite Newspapers

Chameleone Anavyotibuana na Rais Museveni

0

HIVI karibuni nchini Uganda kwenye uwanja wa siasa, Waganda wamelipokea jina jipya kutoka katika tasnia ya burudani, safari hii ni Joseph Mayanja, maarufu kama Jose Chameleone ambaye ni mwanamuziki maarufu wa nchi hiyo aliyetangaza nia ya kutaka kuwania kiti cha Meya wa Jiji la Kampala katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021.

 

Haijasahaulika kuwa msanii huyo aliyewahi kutamba Afrika Mashariki na ngoma za kuvutia kama ‘Shida za Dunia’ na “Wale Wale’, alikuwa akihusishwa na mpango wa kugeukia siasa kwa muda mrefu, lakini mara zote zilionekana kuwa ni habari za uzushi.

 

“Nilianza kuwa na mpango wa kuwa meya tangu mwaka 2005. Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa meya mwenye umri mdogo zaidi katika Jiji la Kampala,” anasema Chameleone katika mahojiano na Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC).

 

“Nimekuwa kiongozi kwa maisha yangu yote, hivyo haitakuwa changamoto kwangu kuwaongoza watu wa Kampala ikiwa watataka nifanye hivyo, niwe Meya wao.”

Ifahamike kuwa Chameleone mwenye umri wa miaka 40 sasa ni mwendelezo wa wimbi la wasanii waliouvamia ulingo wa siasa katika miaka ya hivi karibuni duniani.

 

Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati nao umewahi kuwashuhudia wasanii wengi wakifanya hivyo, ikitosha kuwataja Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’ wa Uganda, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ na Joseph Mbilinyi ‘Mr. Sugu’, hawa ni wasanii wa muziki wa kizazi kipya waliojitosa kwenye siasa.

 

Sugu anawakilisha Jimbo la Mbeya Mjini na Profesa J ni mbunge wa Jimbo la Mikumi, Morogoro. Afande Sele naye alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2015 Jimbo la Morogoro Mjini lakini hakufanikiwa.

 

Miezi miwili iliyopita, Ukraine ilishuhudia mwigizaji Volodymyr Zelensky (41) akiukwaa urais, tena kwa kishindo, akizoa asilimia zaidi ya 70 dhidi ya kiongozi aliyemaliza muda wake, Petro Poroshenko, aliyeambulia asilimia 24 pekee.

Tafiti zimebaini kuwa ushiriki wa vijana katika kuziwania nafasi mbalimbali za kisiasa umeongezeka, sababu kubwa ikiwa ni wengi wao kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda kwenye nchi zao na serikali zao.

 

Juu ya kilichomvuta Chameleone kujitosa ulingoni safari hii, anasema ni kutokana na kuzorota kwa huduma za serikali kuhudumia jamii.

Baada ya kuanika kuwa atajiunga na upinzani kwa tiketi ya Democratic Party (DP), ukweli ni kwamba ameongeza presha kubwa kwa Rais Yoweri Museveni wa chama tawala, National Resistance Movement (NRM).

 

Ikumbukwe kuwa Rais Museveni anajiandaa kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu ujao baada ya kufanikisha mabadiliko ya Katiba yaliyoondosha kipengele cha ukomo wa umri kugombea urais.

Awali, Katiba ya Uganda ilitamka wazi kuwa ukomo wa kiti cha urais ni miaka 75, hivyo ilimweka kando Rais Museveni (73) katika uchaguzi ujao.

 

Tukirejea kwa mwanamuziki Chameleone, kwa muda mrefu amekuwa na uhusiano mzuri na Rais Museveni. Hata kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, alikutana na Rais Museven katika kuandaa mpango wa kampeni.

 

Chanzo kilichokuwa katika kikao hicho kilisema mwanamuziki huyo aliahidi kumuunga mkono Rais Museven na NRM katika uchaguzi huo.

Kampeni zilipoanza, ikikumbukwa kuwa Bobi Wine aligoma, Chameleone aliwaongoza wasanii wengine kutumbuiza katika kila jukwaa kwa lengo la kumnadi Rais Museven.

 

Ni kipindi ambacho baadhi ya mashabiki wa mwimbaji huyo waligomea matamasha yake kuonesha kukerwa kwao na ushiriki wake katika kampeni hizo.

Lakini sasa, uwadui kati ya Rais Museveni na Chameleone ulianza ghafla hivi karibuni, siku chache baada ya msanii huyo kutangaza nia ya kuingia katika siasa.

 

Katika kile ambacho hakikutarajiwa na wengi, Rais Museveni aliacha ‘kum-follow’ msanii huyo kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, ikionesha kuwa ni mwanzo wa kupotea kwa ukaribu wao kutokana na mgongano wa masilahi ya kisiasa.

Kabla ya hapo, Chameleone alikuwa mmoja kati ya watu 24 tu ambao Rais Museveni alikuwa ‘amewa-follow’, mwingine akiwa ni msanii mwingine, Bebe Cool waliyekuwa naye katika kampeni za uchaguzi uliyopita.

 

Aidha, hilo la Chameleone linakuja huku baada ya Rais Museven aliyekaa madarakani kwa miaka 33 akiumizwa kichwa na mwanamuziki na mwanasiasa mwingine kijana, Bobi Wine.

Bobi Wine amekuwa kaa la moto kwa Rais Museveni, akiwataka wananchi wa Uganda kutumia mfano wa kilichotokea Sudan na Algeria kuwaondoa marais waliokuwa wamekaa madarakani kwa muda mrefu.

 

Ikiwa ni miaka miwili tu tangu alipotia mguu katika siasa za upinzani nchini Uganda, Bobi Wine amejikuta akiandamwa na mkono wa Serikali ya Rais Museveni.

Kutokana na msukumo mkubwa alionao kwa vijana, imeshuhudiwa mara kadhaa Rais Museveni akitumia vyombo vya dola kumpa kashikashi mbunge huyo, sambamba na mwenzake wa upinzani, Dk. Kizza Besigye.

 

Moja kati ya matukio ya kushitua ni dereva wake Bobi Wine, Yasiin Kawuma, kuuawa kwa risasi, ukiacha lile la mwanasiasa huyo kupigwa na kisha kwenda Marekani kwa matibabu.

 

Kauli ya hivi karibuni ya Rais Museveni kwamba mwanamuziki anatakiwa kwenda klabu za usiku kuimba na kunengua, inatajwa kuwa ni dalili kiongozi huyo kusumbuliwa na nguvu aliyonayo Bobi Wine katika siasa za Uganda.

 

Bahati mbaya kwake ni kwamba wakati akiwa hajafanikiwa kumzima Bobi Wine, anaibuka Chameleone, ambaye wengi hawaoni kama anatofautiana sana na Bobi Wine linapokuja suala la ushawishi kwa watu hasa vijana.

 

Kulithibitisha hilo, katika moja ya mahojiano yake ya hivi karibuni, Chameleone alifichua kuwa vijana wa bodaboda wamekuwa wakimtaka kugombea kila anapokutana nao. “Nataka kuwa na mchango kama ambavyo Bobi Wine amefanya,” alisisitiza.

 

Kutokana na kazi yao ya muziki, Chameleone akiifanya kwa miaka 20 sasa, ameingia katika siasa akiwa amejikusanyia mtaji mkubwa wa nguvu ya ushawishi wa vijana, ambao kimsingi ndiyo waliombeba Bob Wine kuingia bungeni mwaka 2016.

Ieleweke kuwa vijana ni asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wote wa Uganda, likitajwa kuwa ndilo taifa lenye idadi kubwa ya wananchi wenye umri mdogo.

 

Wakiwa ndiyo wengi zaidi, bado vijana hao hawaoni umuhimu wa Serikali ya Rais Museveni kwa kuwa kama ilivyo katika mataifa mengi ya Afrika, wengi wao wanashinda vijiweni wakiwa hawana kazi, fursa za kiuchumi zikishikiliwa na wachache.

 

Hivyo, haikushangaza kwa Bobi Wine kushinda kiti cha ubunge wa Kyadondo Mashariki katika Uchaguzi Mkuu uliopita akiwa mgombea binafsi mbele ya washindani kutoka NRM na Chama cha Forum for Democratic Change (FDC).

 

Wakimtazama Bobi Wine, kama itakavyokuwa kwa Chameleone, wanawaona kuwa ni wenzao na watazipa kipaumbele changamoto zilizoshindwa na uongozi wa Rais Museveni kwa miaka mingi aliyokaa madarakani.

 

Hata hivyo, kwa uwamuzi wake wa kwenda upinzani, Chameleone anatazamiwa kukumbana na makali ya Rais Museveni katika ulingo wa siasa. Ni kama alivyosema Mwenyekiti wa NRM Mashariki mwa Uganda, Mike Mukula, ambaye amemuonya Chameleone akimtaka kuwa makini na siasa.

 

“Ushauri wangu kwa rafiki yangu kipenzi Chameleon, aende taratibu na siasa. Itakutia umasikini na itapoteza kabisa kipaji chako cha muziki. Usije kusema sikukushauri,” alisema Mukula.

 

Chameleone anakutana na mwanasiasa Museveni ambaye ameshaongoza nchi kwa zaidi ya miongo mitatu.

Bobi Wine amewahi kukiri kuwa anapitia wakati mgumu chini ya upinzani dhidi yake, ikiwa kiongozi huyo na watu wake kupanga kummaliza kiuchumi.

 

“Wanataka niwe na hali ngumu ya kiuchumi,” alisema Bobi Wine akiongeza kuwa baadhi ya waliokuwa akifanya nao kazi ya muziki wamepigwa marufuku kushirikiana naye.

“Viongozi wa serikali ya Uganda wamekuwa wakijaribu kuitangaza picha ya nchi hii kuwa ni yenye demokrasia,” alisema Bobi Wine na kuongeza:

 

“Kwa miaka mingi, haki za watu zimekuwa zikipuuzwa, watu wamekuwa wakiteswa na wengi kuuliwa.”

Tangu alipoanza rasmi kazi ya uwakilishi wa wananchi wake bungeni mwaka juzi, matamasha yake zaidi ya 120 yamefutwa, pigo ambalo huenda likamkuta Chameleone, ambaye ameweka wazi mpango wake wa kuendelea na muziki hata baada ya kuwa Meya.

 

Licha ya Chameleone kusema hajaingia katika siasa kwa ajili ya kuwa kiongozi wa uhasimu dhidi ya serikali au kumtukana rais, kauli yake ya awali, kuwa amejitosa baada ya kuona huduma za serikali kwa jamii zimedorora, inaweza kuonekana ni ukosoaji wa uongozi wa Rais Museveni.

 

Je, Chameleone ameingia katika orodha ya wanasiasa wengi wa upinzani barani Afrika wanaopishana vituo vya polisi kila uchwao? Jibu litakuja tu baadaye.

Leave A Reply