The House of Favourite Newspapers

Hawa Ndio Waliomsaidia Nyerere Akiwa Hana Kitu – 9

0

BAADA ya kuona urafiki wake Mwalimu Julius Nyerere na mzee Mshume na mzee Ally Sykes na kadhalika; wiki hii tumjadili Oscar Kambona ambaye aliwahi kumuokoa Nyerere asiuawe na askari waasi waliovamia ikulu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

 

Kumekuwa na hulka ya kupotosha ama kwa bahati mbaya, au kwa makusudi, historia na mchango wa baadhi ya marafiki wa Nyerere ambao walikuwa wapigania uhuru wa Tanganyika ambao juhudi zao zilichangia kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

 

Kuna orodha ndefu ya wanamapinduzi na waasisi wa taifa letu ambao hawakumbukwi tena licha ya awali kuwa marafiki wakubwa wa Mwalimu Julius Nyerere, mmoja wao ni Oscar Salathiel Kambona, Katibu Mkuu wa kwanza wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU).

 

Oscar alizaliwa Agosti 13 mwaka 1928 katika kijiji cha Kwambe kilichopo mwambao mwa Ziwa Nyasa, karibu na Mbambabay, Wilaya ya Mbinga (wakati huo), Mkoa wa Kusini ambao baadaye uligawanywa na kuunda mikoa mitatu—Lindi, Mtwara na Ruvuma.

 

Oscar alikuwa mtoto wa Mchungaji David Kambona na mama yake aliitwa Miriam Kambona.

Mchungaji Kambona alikuwa ni miongoni mwa Waafrika wa kwanza kupata upadre katika Kanisa la Anglikana la Tanganyika.

 

Kambona akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo Oscar akawa na hamu sana ya kuitumikia nchi yake.

Oscar alipata elimu ya msingi nyumbani kwao Kwambe, akifundishwa na wazazi wake na wajomba zake wawili ambao wote walikuwa walimu.

 

Baada ya hapo alipelekwa Shule ya Kati ya Mt. Barnabas, Liuli, na baadaye shule ya Sekondari ya Alliance, Dodoma ambako alilipiwa ada na Mzungu ambaye alikuwa ni Askofu wa Anglikana. Kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya mwaka ya Pound za Uingereza 30.

Alimshawishi askofu huyo kumlipia ada baada ya kusema bila kukosea sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni… kwa Kiingereza.

 

Alichaguliwa kwenda Tabora Boys Senior Government School, ambako alikutana na Mwalimu Julius Nyerere kwa mara ya kwanza na kujenga urafiki; wakati huo Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya Kikatoliki ya St. Mary’s Tabora.

 

Baada ya kumaliza masomo ya sekondari, Oscar alienda kufundisha shule aliyopitia ya Alliance, Dodoma na baadaye alichaguliwa kuwa ‘Schoolmaster’.

Walikutana na Nyerere kwa mara ya pili kwenye mkutano wa kitaifa wa walimu mwaka 1954; urafiki wao ukashamiri zaidi, akamshawishi kujiunga na TANU.

 

Oscar Kambona alikubali kukitumikia chama cha TANU ambacho kilikuwa kimeanzishwa muda si mrefu, lakini Nyerere akasema wasingeweza kumwajiri kwa vile chama kilikuwa hakina fedha, akawa anapiga ‘dei waka’, kwamba jioni wenye fedha wanamchangia hela ya kula.

Oscar Kambona akasema chama hakikuwa na fedha, kwa vile hakikuwa na ‘Katibu Mipango na Oganizesheni, na ndipo alipoamua kufanya kazi hiyo bila ya mshahara.

 

Aliishi kwa miezi sita akitegemea akiba yake na fadhila za marafiki akiwemo Nyerere.

Katika kipindi hicho, Oscar Kambona alisafiri sehemu mbalimbali za Tanganyika na kuonana na machifu na wazee wa vijiji kusajili wanachama wapya wa TANU.

 

Katika miezi sita alifanikiwa kusajili wanachama 10,000, na kwa mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000.

Oscar Kambona alitumia michango aliyopata kufungua akaunti ya kwanza ya TANU. Kisha alienda Butiama kumshawishi rafiki yake Nyerere achukuwe uongozi wa chama moja kwa moja.

 

Baada ya miaka mitatu, Oscar Kambona aliamua kwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle Temple, nchini Uingereza mwaka 1957 kwa ufadhili wa gavana.

Oscar Kambona alichaguliwa kuwa kiongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Tanganyika na Mwenyekiti wa Tawi la TANU la London akawa anawasiliana sana na Nyerere.

 

Akiwa Uingereza, Oscar Kambona alikuwa Mwafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya habari kwa Kiswahili katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC.

Urafiki wao uliendelea kwa kufa na kupona, mikikimikiki na hatari nyingi,

Je, uliendeleaje? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply