The House of Favourite Newspapers

SIMANZI! BI HARUSI AFARIKI DUNIA GHAFLA AKISUBIRI NDOA

PANGA maisha uwezavyo, lakini mpangaji mkuu atabaki kuwa Mungu aliyeshika uhai wako kama ambavyo msichana mmoja jijini Dar es Salaam aliyekuwa akisubiri ndoa yake kujikuta akifariki dunia ghafla, Uwazi lina mkasa mzito wa kusikitisha. 

 

Msichana huyo aliyejulikana kwa jina la Doris Christiandus (35), mkazi wa Kijitonyama ambaye taratibu zote za harusi zilikuwa zimekamilika, amefariki dunia hivi karibuni na kwamba ndoa yake ilikuwa ifungwe Juni 18 mwaka huu baada ya kufanyiwa sherehe ya kuvishana pete ya uchumba.

 

SIMULIZI INAANZA

Akizungumza kwa uchungu rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Bernadeta alisema kuwa, kabla ya kufikwa na umauti, Doris alikuwa hasumbuliwi na tatizo lolote la kiafya.

 

Ukisikia simulizi hii; rejea kauli ya: “Hakuna ajuaye siku wala saa ya kifo chake,” ambayo imebeba ujumbe kuwa si lazima uugue ndiyo ufariki dunia, kifo kinaweza kukutokea kama kilivyofanya kwa Doris. “Alikuwa haumwi, alikuwa na furaha na mtu aliyeisubiri kwa hamu siku yake ya ndoa, lakini ghafla alianza kulalamika kubanwa na kifua mwisho wake akapoteza maisha,” alisema rafiki wa marehemu.

DORIS ALIVYOPIGANIA UHAI

Inaelezwa kuwa, baada ya bi harusi huyo kuanza kulalamikia maumivu ya kubanwa kifua, aliomba kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Kairuki iliyopo Victoria, wilayani Kinondoni jijini Dar. “Mchumba wake ndiye alimpeleka hospitalini usiku akapumzishwa, lakini kwa bahati mbaya kesho yake alifariki dunia,” alisema rafiki huyo.

 

MATARAJIO YA HARUSI YALIVYOKUWA

Mmoja kati ya wanakamati waliokuwa wakishughulikia maandalizi ya harusi ya Doris alisema kuwa, ilikuwa ifanyike katika viwango vizuri hasa kutokana na mipango mingi kukamilika. “Send off yake ilikuwa ifanyike tarehe 16 Juni mwaka huu na harusi tarehe 18 Juni mwaka huu kwa sababu sherehe ya kuvalishana pete ilishafanyika na ilikuwa ya kuvutia sana.

 

“Taratibu zote zilishafanywa mpaka ukumbi ulipatikana, chakula na vitu vyote vilikuwa vimeshalipiwa, leo unapoambiwa Doris hayupo duniani inasikitisha sana,” alisema mmoja wa wanakamati wa harusi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

 

PADRI, MC WA NDOA WAGEUKA WA MSIBA

Katika hali iliyowahuzunisha watu wengi mshereheshaji (MC) aliyekuwa amepangwa kwa ajili ya siku ya ndoa ndiyo aligeuka kuwa MC siku ya msiba wa bi harusi Doris.

 

Aidha, Padri wa Kanisa Katoliki aliyekuwa amepangwa kufungisha ndoa ya Doris na mumewe aliyejulikana kwa jina moja la James ndiye aliyeongoza ibada ya mazishi ya bi harusi mtarajiwa aliyeaga dunia. Tukio hilo lilikuwa kama kugeuza shilingi kutoka kweye sura ya furaha kuwa ya huzuni ambapo waombolezaji wengi walibubujikwa na machozi huku wengine wakiagua vilio.

BWANA HARUSI ALIZA WENGI

Kutokana na uso wa huzuni aliokuwa nao bwana harusi siku ya msiba wa mchumba wake Doris aliyemwacha dunia mpweke wengi walimsikitikia na kumfajiri. Baadhi walishindwa kuzuia hisia zao baada ya bwana harusi kutokeza msibani akiwa anasukuma jeneza lililokuwa limebeba mwili wa mchumba wake na kujikuta wakiangua kilio.

 

DORIS AZIKWA KWA HESHIMA

Baada ya taratibu za kuaga mwili wa marehemu Doris kukamilika jijini Dar, mwili wake ulisafirishwa hadi nyumbani kwao Songea kwa ajili ya mazishi ambako ulizikwa kwa heshima zote.

 

MICHANGO YA HARUSI GIZANI

Kwa kawaida harusi nyingi za Kibongo zimekuwa zikifanyika baada ya kushirikisha michango ya ndugu na jamaa ambao mwisho wa siku hualikwa kwa ajili ya sherehe jambo ambalo kwa Doris limeshindwa kutimia. Uzoefu unaonesha kuwa endapo harusi haikufanyika kwa sababu za kibinadamu siyo za Kimungu kama kifo baadhi ya wachangaji hujitokeza kutaka warudishiwe fedha zao.

 

Uwazi lilipododosa itakuwaje juu ya wale waliochanga fedha zao; swali lilikosa jibu kutokana na wahusika wa sherehe iliyovunjika kuwa katika kipindi cha majonzi makubwa.

 

Kama hilo la michango halitoshi katika harusi nyingi kumekuwa na sintofahamu ya fedha za malipo ya awali ya ukumbi, MC, vinywaji, mavazi, chakula na gharama zingine kutorudishwa endepo sherehe itavunjika kibinadamu ambapo kwa hili, Uwazi linawaomba waliohusishwa kwenye shughuli ya harusi ya Doris wawe na moyo huo wa ubinadamu.

 

Aidha, shukrani za kipekee zimuendee mwandishi Flora Lauwo wa Nitetee Foundation kwa upatikanaji wa habari hii ya kusikitisha. Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu.

Comments are closed.